Siasa

ODM yamwomba Kikwete majeshi

MBUNGE wa chama cha ODM kinachoongozwa na Bw. Raila Odinga nchini Kenya, Bw. Mohammed Dor Mohammed, amemwomba Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), Rais Jakaya Kikwete, kupeleka kikosi cha kulinda amani nchini humo, ili kunusuru vurugu za kisiasa na mauaji ya kikabila yanayoendelea.

Na Gladness Mboma

 

MBUNGE wa chama cha ODM kinachoongozwa na Bw. Raila Odinga nchini Kenya, Bw. Mohammed Dor Mohammed, amemwomba Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), Rais Jakaya Kikwete, kupeleka kikosi cha kulinda amani nchini humo, ili kunusuru vurugu za kisiasa na mauaji ya kikabila yanayoendelea.

 

Bw. Mohammed alitoa ombi hilo jana Dar es Salaam, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Mtaa wa Mafia, Kariakoo, akifuatana na Bw. Hassan Omar, ambaye ni Mweka Hazina wa Jukwaa la Kitaifa la Viongozi wa Kiislamu Kenya na viongozi wengine wa Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania.

 

Mbunge huyo ambaye alikuwa akizungumzia mtazamo wa Waislamu wa Kenya kuhusu hali ya kisiasa nchini humo, alisema Wakenya wameifurahi baada ya kusikia kuteuliwa kwa Rais Kikwete kuwa Mwenyekiti wa AU.

 

“Tuna imani Rais Kikwete ataingilia kati masuala ya Kenya ili kuleta amani, kwa sababu ni moja ya majukumu yake na ni mtihani mkubwa kwake, tunamsikitikia kwa kuwa ameingia na kukuta kazi ngumu ya kuingilia nchi yenye mzozo wa kisiasa na kikabila,” alisema Bw. Mohammed.

 

Alisema chanzo hasa cha mgogoro na mauaji yanayotokea Kenya ni Tume ya Uchaguzi nchini humo (ECK) kutangaza matokeo ya urais kinyume na ilivyokuwa, hivyo aliiomba AU kuingilia kati ili kuleta amani haraka.

 

Bw. Mohammed alisema Wizara inayoshughulikia usalama nchini humo, imeshindwa kutekeleza majukumu yake na kwamba mauaji yanayotokea yanatokana na askari kuua raia.

 

“Wananchi wanapofanya maandamano ya amani ambayo yamekubaliwa na mataifa ya nchi zote duniani, Wizara ya Usalama Kenya inapinga maandamano hayo na kuua wananchi ovyo … ni chanzo kikubwa cha vurugu na mauaji nchini,” alisema Bw. Mohammed.

 

Alisema kikosi cha kulinda amani cha AU kinatakiwa kuingia Kenya haraka na kwamba Bw. Kikwete asisubiri idadi ya vifo iongezeke na kwamba hawataki nchi hiyo iwe kama Chadi.

 

Aliongeza kuwa wakiwa viongozi wana imani na mazungumzo yanayoendelea ambayo yanaongozwa na Katibu Mkuu mstaafu wa Umoja wa Mataifa, Bw. Kofi Annan.

 

Alisema iwapo Rais Mwai Kibaki na Bw. Odinga wataondoka katika meza ya mazungumzo watambue kuwa vifo vitaendelea na roho za Wakenya zinazopotea zitawasuta kwa Mungu.

 

“Wakati mazungumzo yakiendelea naomba kusiwe na maneno ya chuki kutoka pande zote mbili kwa sababu hizo ndizo zinazozua chuki,”alisisitiza Bw. Mohammed

 

Alisema ukabila Kenya umepita kiasi na kwamba nyumba za ibada zilizochomwa moto hazikukusudiwa, bali wananchi waliokuwa wamekimbilia kujihifadhi humo.

 

Wakati huo huo, Amir wa Shura ya Maimamu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kikao cha Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Shekhe Mussa Kundecha, alidai kupata habari ya kukamatwa kwa Wakenya 70 walioingia nchini na kupelekwa katika magereza ya Segerea na Keko, Dar es Salaam.

 

Alidai kuwa kati ya wakimbizi hao, mmoja ni mwanamke ambaye amejifungulia gerezani na viongozi wamepanga kwenda kuwajulia hali na kuangalia matatizo waliyonayo mara baada ya kumaliza kikao chao.

 

Bw. Kundecha alidai kuwa Wakenya waliokimbilia Zanzibar kuwa walipokewa vizuri na kupewa hifadhi nzuri.

 

Source: Majira

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents