Habari

Ofisi ya Makamu wa Rais kuja na ajenda ya kuifanya Dodoma kuwa ya kijani

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema ataanza kampeni rasmi ya kuifanya Dodoma kuwa ya kijani tarehe 21 ya mwezi huu kwa kupanda miti katika mji huo.

Makamu wa Rais ameyasema hayo leo wakati wa hafla fupi ya kumkaribisha rasmi mkoani Dodoma ambapo atakuwa akiishi na kufanya majukumu yake ikiwa sehemu ya azma ya Serikali ya awamu ya Tano ya kuifanya Dodoma Makamo Makuu ya Nchi.

Makamu wa Rais alitoa shukrani za dhati kwa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa kumrahisishia kuhamia Dodoma pamoja na Waziri Mkuu .

“Tupo Dodoma na Tumehamia rasmi Dodoma, Mwaka mmoja na nusu sasa toka tamko la kuhamia Dodoma limetolewa kuwa ile safari ya Kanani kwa upande wangu leo imetimia”

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa aliielezea siku ya leo kuwa ni siku ya furaha kubwa kwa Watanzania wote haswa wakazi wa Dodoma.

Waziri Mkuu alimuhakikishia Makamu wa Rais kuwa Dodoma ni nzuri, na wana Dodoma wamefarijika sana na sekta za utoaji huduma za jamii zimetanuliwa.

Waziri Mkuu alisema kuwa Dodoma ni rahisi kufikika na wananchi kutoka kona zote za nchi yetu, hivyo fursa zipo nyingi kwa wananchi wa Dodoma na wa mikoa ya jirani.

Waziri Mkuu alianisha barabara kadhaa ambazo zimekamilika kwa kiwango cha lami na zinazorahisisha usafiri kufika Dodoma lakini pia alizungumzia mradi wa reli mpya ya Standard Gauge ambayo itasaidia usafiri kwa muda mfupi kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam.

Katika hafla hiyo fupi iliohudhuriwa pia na Mawaziri mbali mbali akiwemo Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe.January Makamba, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Mhe. Jenister Mhagama, Waziri wa Katiba na Sheria Profesa Palamagamba Kabudi na Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Harrison Mwakyembe, pia Viongozi wastaafu balozi Lusinde na Mzee Ndenjembi walikuwepo kushuhudia Makamu wa Rais kuhamia Dodoma ambapo walimpa jina la kiasili la Mbeleje hivyo Mama Samia hapa Dodoma atafahamika kwa Mama Mbeleje pia.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents