Habari

Onyo la Marekani laiogopesha Ugiriki, yajiweka mbali na meli ya Iran

Ugiriki imekataa kuisaidia meli ya mafuta ya Iran ambayo hivi majuzi ilizuiliwa Gibraltar kwa tuhuma ya kusafirisha mafuta kuelekea Syria.Meli inayopeperusha bendera ya Iran

Meli hiyo iliondoka Gibraltar siku ya Ijumaa

Naibu waziri wa maswala ya kigeni Miltidias Varvitsiotis aliambia chombo cha habari cha ANT 1 kwamba taifa lake haliko tayari kuisaidia Meli hiyo inayodaiwa kuelekea Syria.

Hatua hiyo inajiri baada ya waziri wa maswala ya kigeni nchini Marekani Mike Pompeo kutishia vikwazo dhidi ya taifa lolote ambalo litaisaidia meli hiyo.

Adrian Darya 1 iliondoka Gibraltar siku ya Jumapili na kusema kwamba inaelekea katika bandari ya Ugiriki ya Kalamata.

Mamlaka katika taifa hilo linalomilikiwa na Uingereza iliizuia meli hiyo mwezi Julai. Awali ilijulikana kama Grace 1.

Licha ya ombi la dakika za mwisho la Marekani , Gibraltar iliiwachilia meli hiyo siku ya Ijumaa na meli hiyo ikaondoka na kuelekea mashariki mwa bahari ya Mediterenea.

Iran ilinukuliwa ikisema kwamba iko tayari kutuma wanamaji wake ili kuisindikiza meli hiyo na sasa iko kaskazini mwa bandari ya Algeria ya Oran.

Je Ugiriki imesemaje?

Kulingana na vyombo vya habari vya taifa hilo, bwana Varvitsiotis alithibitisha kwamba Marekani imeitaka kutoisaidia meli hiyo.

Iran haijawasiliana na serikali ya Ugiriki, alisema.

Hatahivyo meli hyo ya Adrian 1 ambayo inabeba mapipa milioni 2 ya mafuta ghafi ni kubwa mno kwa bandari yoyote ya Ugiriki kuiegesha, alisema bwana Varvitsiotis.

Alipoulizwa je Ugiriki itachukua hatua gani iwapo meli hiyo itaegesha katika maji ya taifa hilo, alijibu iwapo hilo litatokea tutaona la kufanya.

Marekani inaamini Adrian Darya-1 ina uhusiano na jeshi la Iran la Revolutionary Guard – tawi la jeshi la taifa hilo ambalo limetajwa kuwa kundi la kigaidi na Marekani.

”Tunataka kuwanyima njia za kuendeleza kampeni yao ya ugaidi” , bwana Pompeo aliambia maripota.

”Tumesema wazi kwamba mtu yeyote atakayeisaidia , yeyote atakayeiruhusu kuegesha katika bandari yake atakuwa katika hatari ya kupokea vikwazo vya Marekani”, alisema akiongezea Marekani itachukua hatua inayoweza kuizuia meli hiyo kuwasili Syria.

Je meli hiyo inaelekea wapi?

Adrian Darya-1 bado imesema kwamba inaelekea katika bandari ya Kalamata

Samir Madani, mwanzilishi wa tovuti ya maswala ya baharini TankerTrackers.com, ameambia BBC kwaba meli hiyo ilikuwa inajaribu kurudi nyumbani kupitia rasi ya Suez Canal.

Italazimika kupakua mapipa milioni moja kwa meli nyengine ambayo itakuwa ikipeperusha bendera ya Iran kwa kuwa meli hiyo imebeba uzani mkubwa, alisema.

Kuelekea Syria pia itakuwa vigumu kwa kuwa imebeba mafuta mengi mno kupakua bila usaidizi katika bandari ya Baniyas.

Meli hiyo ilichukua njia ya mviringo kuelekea Mediterrenia , ikisafiri kwa kuizunguka Afrika badala ya kuchukua njia fupi ya rasi ya Suez canal.

”Sio lazima wazunguke njia yote hiyo ili kuwasili Syria”, alisema bwana madani.

Kwa mujibu wa shirika la habari la BBC, Wachanganuzi wanaamini kwamba meli hiyo inaelekea katika maji ya Syria kama eneo salama , na kutokea hapo watapakua mafuta kwa meli ndogo ndogo kupeleka katika maeneo ya Meditereania.

Inaweza kuwa wanunuzi wa kusini mwa Ulaya kwa mfano , alisema.

Je kuna mgogoro gani wa meli hiyo ya mafuta?

Meli hiyo na wafanyakazi wake 29 kutoka India, Urusi, Latvia na Ufilipino ilikamatwa na wanamaji wa Uingereza tarehe 4 mwezi Julai baada ya serikali ya Gibraltar – eneo linalomilikiwa na Uingereza kusema kwamba inaelekea Syria swala ambalo ni ukiukaji wa vikwazo vya Muungano wa Ulaya.

Hatua hiyo ilizua mgogoro wa kidiplomasia kati ya Uingereza na Iran ambao uliendelea kwa wiki kadhaa huku nayo Iran ikilipiza kisasi kwa kuikamata meli ya Sweden iliokuwa ikipeperusha bendera ya Uingereza Stena Impero katika Ghuba.

Stena Impero bado ipo katika maji ya Iran ikiendeleza kuzuiliwa.

Kumekuwa na uvumi kwamba meli hiyo itaachiliwa iwapo Adria Darya itaachiliwa licha ya maafisa kukana habari hizo.

Msemaji wa wizara ya maswala ya kigeni alisema siku ya Jumatatu kwamba walikuwa wakisubiri agizo la mahakama kabla ya meli hiyo kuachiliwa lakini wakasema kwamba hakuna uhusiano wowote wa meli hizo mbili.Ramani inayoonyesha njia iliotumiwa na meli hiyo baada ya kukamatwa Gibraltar

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents