Habari

‘Osama’ amkera Lowassa Dodoma

WAZIRI Mkuu, Edward Lowassa, ameliagiza Jeshi la Polisi wilayani Mpwapwa, Dodoma, kumkamata Mwenyekiti wa Kijiji cha Kibakwe, Laurian Ngingo ‘Osama’ kwa tuhuma za kuhujumu mali za kijiji.

na Peter Nyanje, Mpwapwa


WAZIRI Mkuu, Edward Lowassa, ameliagiza Jeshi la Polisi wilayani Mpwapwa, Dodoma, kumkamata Mwenyekiti wa Kijiji cha Kibakwe, Laurian Ngingo ‘Osama’ kwa tuhuma za kuhujumu mali za kijiji.


Waziri Mkuu, aliamuru kukamatwa kwa Osama na kumfikisha mahakamani kwa tuhuma hizo.


Lowassa alitoa agizo hilo juzi, wakati akihutubia mkutano wa hadhara kijijini hapo, kutokana na malalamiko ya wakazi hao, ambao walimweleza licha ya tuhuma nyingi zinazomkabili, kiongozi huyo bado anatamba mitaani akitoa maneno ya kashfa na matusi kwa viongozi wengine.


Osama, anatuhumiwa kutoa lugha ya matusi dhidi ya Mkuu wa Wilaya (DC) ya Mpwapwa, Halima Dendego na kumkataza Mbunge wa Jimbo hilo, George Simbachawene, kufanya mikutano katika eneo hilo bila idhini yake.


Aidha, kiongozi huyo wa kijiji, amefungua kesi ya madai dhidi ya Dendego, akitaka kulipwa vitu mbalimbali vyenye thamani ya takribani sh milioni saba.


Akizungumza katika mkutano wa hadhara, mkazi mmoja wa Kibakwe, Makelele Mwaluke, alimweleza Waziri Mkuu kuwa, Ngingo anatuhumiwa kuiba mabomba yaliyoletwa kwa ajili ya mradi wa maji.


“Sisi tunashangaa huyu ni Osama gani? Mbona Osama bin Laden anatafutwa na (rais wa Marekani George) Bush?” alihoji mwanakijiji huyo huku akishangiliwa na wenzake.


Mwanakijiji mwingine, Fulgence Kasege alidai mwenyekiti huyo amechukua bila idhini, sh milioni tatu za Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT).


Aidha, Kasege alidai pia Osama alighushi mihtasari wa mkutano pamoja na kuandaa watia saini bandia na kufanikiwa kuchota sh 500,000 kutoka katika akaunti ya kijiji iliyokuwa na sh 1,150,000.


Baada ya kusikia madai hayo, Lowassa alishangaa na kuwahoji wananchi hao kwa nini wanaendelea kumuachia Osama huyo akitamba kijijini bila kumchukulia hatua.


“Mna polisi hapa?” alihoji Lowassa na kujibiwa kuwa wapo. Baada ya kusikia hivyo, aliwaagiza polisi kukusanya ushahidi kuhusu tuhuma zinazomkabili mwenyekiti huyo na kumfikisha mahakamani.


Hata hivyo, wananchi hao walimweleza Waziri Mkuu kuwa, walishafikisha malalamiko yao kwa Mkuu wa Wilaya, lakini alipokuja hapo, mwenyekiti huyo anadaiwa kukataa kuonana naye huku akisema kuwa hatishwi na mtu anayevaa sketi.


“Huyu kiongozi gani anatishia mpaka DC? Vyombo vya dola vinawajibika kumlinda DC, iwapo DC hatolindwa na vyombo vya dola, nani atamlinda?” alisema Lowassa na kuhoji.


Baadaye, akisimulia mikasa ya mwenyekiti huyo, Simbachawene alisema kuwa ni mtu ambaye anamiliki kilabu cha pombe za kienyeji katika eneo hilo na amekuwa ‘akiwasumbua’ mno nyakati za uchaguzi.


Alisema Ngingo alikuwa mwalimu, kabla hajasimamishwa kutokana na matatizo mbalimbali, naye akaamua kujitosa katika siasa na kugombea udiwani kupitia CCM.


“Lakini alishindwa katika kura za maoni kwa kura mbili. Akahamia CHADEMA ambako alitupa shida sana, lakini nako alishindwa. Baada ya uchaguzi huo, ikatokea nafasi ya mwenyekiti wa kijiji naye aliamua kurudi CCM na kuwania nafasi hiyo,” alisema.


Katika kura za maoni, Ngingo alipata zaidi ya 400 huku mtu aliyemfuatia akipata 54 na hapo ilibidi apitishwe kuwania uenyekiti huo ambao aliupata.


Simbachawene alisema ni kweli mwenyekiti huyo aliwahi kumuandikia barua, akimtaka kutofanya mikutano katika eneo hilo bila ya kupata idhini yake na kuisaini chini kama Gavana.


Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents