Habari

OSHA imechangia kupunguza ajali sehemu za kazi – DC Mkuranga  (+Video)

Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Filbert Sanga, amesema ukaguzi pamoja na elimu inayotolewa na Mamlaka ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) vimechangia kwa kiwango kikubwa kupunguza ajali katika sehemu za kazi katika wilaya yake.

Mhe. Sanga ameyasema hayo alipofanya ziara katika ofisi za OSHA za jijini Dar es Salaam kwa lengo la kujifunza jinsi taasisi hiyo ya umma inavyotekeleza majukumu yake ambayo yanalenga kulinda afya ya mfanyakazi pamoja na mali za wawekezaji ili kuleta tija katika uzalishaji.

Kwa upande wake, Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda amemshukuru Mkuu wa Wilaya huyo kwa kutambua mchango wa taasisi yake katika kuchochea maendeleo ya Wilaya ya Mkuranga na Taifa kwa ujumla.

Awali, viongozi hao wawili walikuwa na kikao kifupi ambapo walibadilishana mawazo juu ya namna ambavyo taasisi ya OSHA inaweza kushirikiana na ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga katika kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi katika wilaya hiyo yenye viwanda vikubwa zaidi ya 90 pamoja na shughuli nyinginezo nyingi za kiuchumi.

OSHA ni taasisi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu yenye jukumu la kuhakikisha kwamba wafanyakazi wanafanya kazi katika mazingira salama ili kuepuka ajali na magonjwa yatokanayo na kazi.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents