Habari

Padri ahukumiwa kifungo cha maisha jela

MAHAKAMA ya Rufaa ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) imebatilisha adhabu ya kifungo cha miaka 15 jela aliyopewa awali Padri wa zamani wa Kanisa Katoliki nchini Rwanda, Bw. Athanas Seromba na kumhukumu kifungo cha maisha jela kwa muda uliosalia wa maisha yake.

Na Nicodemus Ikonko wa Hirondelle, Arusha

 

 

 

MAHAKAMA ya Rufaa ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) imebatilisha adhabu ya kifungo cha miaka 15 jela aliyopewa awali Padri wa zamani wa Kanisa Katoliki nchini Rwanda, Bw. Athanas Seromba na kumhukumu kifungo cha maisha jela kwa muda uliosalia wa maisha yake.

 

Jaji Mohamed Shahabuddeen aliyekuwa anaongoza jopo la majaji watano wa Mahakama hiyo jana alisema idadi kubwa ya jopo lake walikubaliana kumpa adhabu ya kifungo cha maisha jela kwa muda wote uliobakia wa maisha yake.

 

Alifafanua, kwamba kitendo cha Padri Seromba kukubaliana na viongozi wa Serikali za mitaa kutumia tingatinga kubomoa Kanisa huku akijua wazi ndani yake kuna wakimbizi wa kitutsi wapatao 1,500 na kwamba wangepoteza maisha, kilifanya majaji hao kukubaliana kwa kauli moja kwamba alisaidia kutendeka kwa mauaji ya kimbari na kuteketeza kizazi.

 

Sambamba na hoja hiyo, majaji hao pia walimtia hatiani kwa kusaidia kuuawa kwa Watutsi wengine wawili, kuwatimua kazi wanne waliokuwa wanafanya kazi katika Parokia yake na kukataa kuendesha ibada iliyoombwa na Watutsi waliokuwa wanapata hifadhi katika Kanisa hilo.

 

Kama vile hayo hayatoshi, Mahakama ya Rufaa pia iliridhika kwamba Padri Seromba aliwazuia wakimbizi wa kitutsi kujitafutia chakula katika shamba la migomba lililokuwa jirani na Kanisa hilo.

 

“Kwa nafasi aliyokuwa nayo katika jamii, Padri Seromba alitenda makosa ya mauaji ya kimbari na kuteketeza kizazi,” alisema Jaji.

 

Padri Seromba akiwa amesimama mahakamani jana wakati hukumu hiyo ikisomwa alionekana na sura ya huzuni wakati wote.

 

Wakili wake, Bw. Patrice Monte alipoulizwa juu ya hukumu hiyo dhidi ya mteja wake, alisema “hii ni taarifa mbaya, majaji hawakuzingatia hoja zote nilizowasilisha katika utetezi wa mteja wangu.”

 

Tofauti na Wakili huyo, Naibu Mwendesha Mashitaka wa ICTR, Bw. Bongani Majola kwa upande wake aliielezea hukumu hiyo kutenda haki na kwamba Padri alistahili adhabu aliyopewa.” Hukumu ya awali ilitolewa na ICTR Desemba 13, 2006.

 

Padri Seromba wakati wa mauaji ya kimbari mwaka 1994 alikuwa Paroko wa
Parokia wa Kanisa Katoliki la Nyange, Kaskazini Magharibi mwa Rwanda.

 

 

 

Source: Majira

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents