Soka saa 24!

Picha: Mrithi wa Dk Kimei CRDB, Abdulmajid atangaza mbinu za kuipaisha benki hiyo!

Mkurugenzi Mtendaji Mpya wa Benki ya CRDB Ndugu Abdulmajid Mussa Nsekela amewahakikishia Wateja, Wanahisa  na Wadau wote wa Benki ya CRDB kuwa Benki hiyo ipo kwenye mikono salama na itaendelea kukua pamoja na kuzalisha faida kama ilivyotarajiwa. Bwana Nsekela aliyasema hayo katika Mkutano na Waandishi wa habari wenye lengo la kumtambulisha rasmi uliofanyika katika hoteli ya Serena Jijini Dar es Salaam.


Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela akizungumza na waandishi wa habari, kuelezea mipango na mikakati ya Benki hiyo katika mkutano uliofanyika kwenye hoteli ya Serena, Jijini Dar es salaam, Oktoba 10, 2018.

Akielezea kuhusu vipaumbele vyake, Ndugu Abdulmajid Mussa Nsekela alisema kuwa kwa kushirikiana na viongozi na wafanyakazi wa Benki hiyo, amedhamiria kufanya maboresho makubwa katika utoaji huduma kwa wateja kwa kutilia mkazo katika maeneo matano muhimu, ambayo ni uboreshaji wa mifumo na taratibu za  utoaji huduma, ili ziendane na mahitaji halisi ya wateja na soko, kuongeza weledi na umahiri wa wafanyakazi, kuwekeza kwenye teknolojia ya kisasa, kukuza biashara katika nyanja zote ili kuendana na kasi ya serekali ya awamu ya tano. Atahakikisha Benki inafanya vizuri na kupata faida zaidi ili kutoa gawiwo nono kwa wanahisa.

“Tutakuwa tukiboresha mara kwa mara taratibu za jinsi ya kupata na  kutumia huduma zetu. Tunataka upatikanaji na utumiaji wa huduma za Benki CRDB  uwe rahisi, huku tukiendelea kusizogeza huduma hizo karibu zaidi na wateja wetu” alisema Ndugu Nsekela.

Akifafanua zaidi juu ya uboreshwaji wa huduma na mikakati ya Benki ya CRDB katika eneo hilo muhimu, Ndugu Nsekela alisema kwa kipindi kifupi kijacho Benki ya CRDB itajikita zaidi kwenye uwekezaji wa mifumo ya kidigitali (innovative products and services) itakayowezesha kuwafikia wateja wengi zaidi, kwa urahisi zaidi, mahali popote walipo na hivyo kuwaondolea wateja wao ulazima wa kutembelea matawi ya Benki ya CRDB pindi wanapohitaji huduma. “Tutatumia fursa ya kuwa zaidi ya watanzania milioni 19.3 wanatumia simu za mikononi kufanya miamala yao na kuwashawishi kutumia bidhaa zetu za SimBanking na SIMAccount ambazo nazo hutoa huduma kama hizo” alisema.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB, Ally Laay akijadiliana jambo na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Abdulmajid Nsekela wakati wa mkutano na waandishi wa habari, uliofanyika kwenye hoteli ya Serena, Jijini Dar es salaam, Oktoba 10, 2018.

Akiongelea kuhusu mikakati ya kusogeza huduma kwa wateja, Ndugu Nsekela alisema Benki ya CRDB imejiwekea malengo ya kufikisha huduma katika wilaya zote nchini ifikapo mwaka 2022. Na wamejiwekea lengo la kuongeza Mawakala wake wa FahariHuduma katika kila kona ya nchi. Ndugu Nsekela alisema pia Benki hiyo pia ina mpango wa kuendelea kupanua wigo wa huduma zake nje ya nchi.

Akielezea kuhusu mahusiano baina ya Benki hiyo na Serikali na wadau wengine, Ndugu Nsekela alisema kuwa Benki ya CRDB inaitambua Serikali kama Mwanahisha wake na mdau mkubwa wa biashara.

“Benki ya CRDB itaendela kuthamini mahusiano mazuri yaliyopo baina yake na Serikali na taasisi zake na tutaendelea kubuni huduma na bidhaa mbalimbali mahususi kwa ajili ya kufikia mahitaji ya Serikali pamoja na wafanyakazi wake mmoja mmoja.

Tunajivunia kuwa mmoja wa wadau wakubwa wa Serikali ili kwa pamoja tuweze kujenga uchumi wa nchi hususani katika kipindi hiki ambacho tunaelekea katika kujenga uchumi wa kati wa Viwanda,” alisisitiza Ndugu Nsekela.

Ndugu Nsekela alimalizia kwa kusema hali ya uchumi nchini inatoa fursa kubwa ya ukuaji kwa mabenki nchini huku akibainisha kuwa Benki ya CRDB itaendelea kutia mkazo katika kuhudumia wateja Wakubwa, Wadogo na wa Kati pamoja na Biashara ya kilimo pamoja na kuwawezesha wawekezaji kwenye sekta ya viwanda ili kujenga Tanzania ya viwanda.

Related Articles

Back to top button
Bongo5

FREE
VIEW