Picha na video za watumiaji wa mitandao ya kijamii kuanza kuchunguzwa, lengo kukamata wakwepa kodi
Serikali nchini Ufaransa imetangaza kuwa mwakani 2019 itaanza kukagua akaunti zite za mitandao ya kijamii nchini humo kwa lengo la kubaini watu wanaokwepa kulipa kodi kupitia mitandao hiyo.
Akielezea mpango huo, Waziri wa Fedha, Hatua na Akaunti za umma wa Taifa hilo, Gerald Darmanin amesema kuwa mpango huo una lengo la kuchunguza kila akaunti ya Mfaransa ili kudhibiti upotevu wa mapato yatokanayo na matangazo yanayowekwa na watumiaji husika.
Akizungumza juzi kwenye kipindi cha kila wiki kinachojadili masuala ya uchumi cha CAPITAL, Darmanin amesema kuwa kuna watu ambao maisha yao ni ya kawaida lakini wanachapisha picha za magari ya kifahari jambo ambalo anaamini kuwa huenda watu hao wanamiliki vitu vya thamani ambavyo havijalipiwa kodi.
“Mamlaka zetu za kodi zitaangalia kama vitu unavyoposti ni vya kwako au maisha unayoishi yanaendana na kipato chako, kwani tunaona watu wengi wanaweka magari ya kifahari ile hali hawana uwezo wa kuyamiliki.“amesema Darmanin.
“Picha na video zote zitakazopostiwa kwenye mitandao ya kijamii zitaenda kwenye database yetu kwa ajili ya kuchunguzwa na itakuwa ni siri kwa mtumiaji husika,”ameeleza Darminan .
Hatua hiyo ya Ufaransa, imekuja ikiwa ni wiki tatu zimepita tangu nchi hiyo ipitishe sheria mpya ya kuongeza njia za ukusanyaji kodi kwa njia ya mtandao.
CHANZO-https://www.nytimes.com/reuters/2018/11/10/business/10reuters-france-taxes-socialmedia.html