Picha

Ofisi ya waziri mkuu kuendelea kuwaendeleza vijana wabunifu nchini

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi,Vijana na Ajira), Anthony Mavunde amesema Serikali itaendelea kuwatunza, kuwatangaza na kuwaendelea vijana wabunifu nchini ili kuwahamasisha kufanya shughuli za ubunifu nchini. 

Aliyasema hayo leo Jijini Dar es Salaam wakati akipokea tuzo ya Mkurugenzi wa kampuni ya Malkia Investment Ltd, Jenifer Shigole aliyoshinda katika tuzo za African Entrepreneurship Awards nchini Morocco.

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Vijana na Ajira Mhe.Anthony Mavunde akipokea cheti alichoshinda Mjasiriamali na Mkurugenzi wa kampuni ya Malkia Investment ltd Bi. Jenifer Shigole katika tuzo za African entrepreneurship Awards zilizofanyika nchini Morocco na kuibuka mshindi wa kwanza na kujishindia mtaji wa dola laki moja na nusu

Katika shindano hilo, Jenifer aliiibuka mshindi wa kwanza katika kipengele cha masuala ya elimu na mazingira na kujishinda mtaji wa dola laki moja na nusu. “Mtakumbuka Mhe. Rais katika hotuba yake ya ufunguzi wa Bunge alituagiza kuwatambua vijana wabunifu na tayari tumewatambua na kuwaendeleza na natoa rai kwa vijana kujitokeza ili waweze kushilikiana na Serikali” Alisema Mavunde.

Mhe.Anthony Mavunde akizungumza na vyombo vya habari kuhusu Tuzo aliyoshinda Mjasiriamali na  Bi. Jenifer Shigole 

Aidha alisema Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana wataikopesha kampuni ya Jenifa ya Malkia Investment Ltd kiasi cha Tsh Milioni 30 ili zisaidie kupanua mradi wake kwa lengo la kuongeza uzalishaji ili bidhaa zake ziwafikie vijana wengi zaidi waishio vijijini.

Mavunde alisema kuwa Serikali imeipatia kampuni hiyo ekari moja ya kiwanja kilichopo Wilayani Kibaha Mkoani Pwani ili kujenga kiwanda cha kutengeneza pedi za kike ambazo ni mkombozi kwa vijana wa kike hasa walio mashuleni.

Mjasiriamali na Mkurugenzi wa kampuni ya Malkia Investment ltd Bi. Jenifer Shigole Bi. Jenifer Shigole akiwaonyesha waandishi wa habari(hawapo pichani) tuzo aliyoshinda nchini Morocco na kufanikiwa kushika nafasi ya kwanza katika kipengele cha masuala ya Elimu na Mazingira na kujishindia mtaji wa dola moja na nusu. Kushoto ni Meneja wa Programu wa kampuni ya Malkia Investment Juma Rajabu

Anaongeza kuwa Serikali pia itamtambulisha kwa vijana waelimishaji wa kitaifa wa stadi za maisha walioandaliwa na Serikali kwa ajili ya kufundisha stadi za maisha katika mikoa ya Kagera,Mwanza, Geita, Simiyu, Dar es salaam, Pwani, Lindi, Mtwara, Morogoro, Dodoma, Singida, Tabora na Manyara .

Kwa mujibu wa Mavunde hatua hiyo imelenga kusaidia vijana wa kike kupata namna bora ya kutumia bidhaa za kampuni hiyo kwa ajili ya kutunza afya zao. Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi hiyo, Jenister Shigole aliishukuru Serikali kwa kutambua mchango wake na vijana wenzake kwa kuona mchango wao katika jamii na kutoa wito kwa vijana wengi kuwa wabunifu wa miradi mbalimbali.

Alisema kiwanda kitachotarajiwa kuanzishwa na kampuni hiyo kitaisaidia kutengeneza ajira na kupunguza uharibifu wa mazingira kwani pedi wanazotengeneza zimetengenezwa kwa pamba tofauti na zingine ambazo zimetengenezwa kwa plastic.

Aidha Shigole ametoa wito kwa vijana wengi zaidi kushiriki kupitia fursa izi za African Entrepreneurship Awards ambayo itawasaidia kimaendeleo kwa kubuni miradi mbalimbali kupitia uwezo na ujuzi walionao.

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Vijana na Ajira Mhe.Anthony Mavunde akipokea Tuzo kutoka kwa Mjasiriamali na Mkurugenzi wa kampuni ya Malkia Investment ltd Bi. Jenifer Shigole aliyoshinda katika tuzo za za African entrepreneurship Awards zilizofanyika nchini Morocco na kuibuka mshindi wa kwanza katika kipengele cha masuala ya Elimu na Mazingira na kujishindia mtaji wa dola laki moja na nusu.Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi Maendeleo ya Vijana Bi.Venerose Mtenga na wa kwanza kushoto ni Meneja wa Programu wa kampuni ya Malkia Investment Juma Rajabu

Picha na Daudi Manongi-MAELEZO

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents