Pinda amaliza mgomo wa TRL

Waziri Mkuu PindaSERIKALI imeingilia kati na kumaliza mgogoro kati ya wafanyakazi na wawekezaji wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) kwa kuamua kubeba mzigo wa kulipa mishahara ya miezi mitano ambayo itagharimu sh. bilioni 3.6

Grace Michael na Joyce Magoti

SERIKALI imeingilia kati na kumaliza mgogoro kati ya wafanyakazi na wawekezaji wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) kwa kuamua kubeba mzigo wa kulipa mishahara ya miezi mitano ambayo itagharimu sh. bilioni 3.6.

Akizungumza na wafanyakazi wa kampuni hiyo Dar es Salaam jana, Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda, alisema Serikali imeamua kulikabili tatizo lililopo sasa ambalo linawaathiri wananchi, hivyo wafanyakazi watalipwa mshahara wa sh. 160,000 waliokubalina na si sh. 80,000 ambazo wamelipwa kwa kipindi hiki.

“Serikali imeamua kubeba mzigo huu kwa muda wa miezi mitano ikiwa ni kuanzia Machi hadi Julai mwaka huu na baada ya hapo, kampuni itaendelea na mzigo wake, mshahara wa Machi utalipwa ndani ya wiki hii na miezi mingine italipwa kila tarehe 20.

“Serikali imeamua kuikopesha kampuni, kwani inaelewa athari ambazo zinaweza kujitokeza ambazo ni kubwa sana, lakini pia kuwatesa wananchi wetu ambao wamesota kwa kipindi kirefu hapa stesheni,” alisema Bw. Pinda.

Aliwataka wafanyakazi na Menejimenti ya TRL kutumia busara katika kutatua matatizo na kama yameshindikana yafikishwe katika ngazi husika na si kutoa uamuzi ambao utaleta athari kwa wananchi.

Bw. Pinda alikiri kuwapo udanganyifu katika kuingia mkataba kati ya Serikali na kampuni hiyo, ambapo kampuni ilielezwa kuwapo kwa injini 92 na badala yake zikakutwa 55 na baadhi zikiwa mbovu.

“Niliposikia hivyo nilishituka na kujiuliza kuwa nani kamdanganya mwenziwe…lakini mbali na hili nakubaliana kuwa kampuni ina matatizo yake na upande wa pili nao bado una matatizo yake, lakini kwa sasa tushughulikie suala la fedha na mengine yataendelea kwenye kamati inayoshughulikia,” alisema Bw. Pinda.

Aliitaka kampuni hiyo kutojiamulia mambo na badala yake ishirikishe ngazi zote wakiwamo wadau, ili kufikia uamuzi sahihi ambao kila mwananchi ataridhika nao na kuondoa migogoro ambayo inajitokeza mara kwa mara.

Bw. Pinda alisisitiza kuwa mchakato mzima wa kukarabati, ununuzi wa injini, mabehewa na kukodi ni lazima zabuni zake zitangazwe na kufuata sheria ya ununuzi na si kampuni kujiamulia kufanya kwa taratibu zingine na hii itasaidia kuleta ushindani utakaoboresha huduma.

Aliisihi kampuni hiyo kutofuta njia za reli zikiwamo za Mpanda, Tanga na Manyoni, kwani huo si uamuzi wa busara kutokana na madhara yake kuwa makubwa hasa kwa wananchi wanaotegemea njia hizo.

Baadhi ya wafanyakazi waliozungumza na Majira walisema mkataba ulioingiwa na shirika unatakiwa kurejeshwa bungeni, ili ujadiliwe kutokana na kujaa mazingira ya rushwa na udanganyifu.

“Mkataba huu una ufisadi wa hali ya juu na bila kupitiwa upya, Serikali itakuwa na kazi ya kukopesha mishahara kila siku na matatizo hayatakwisha katika kampuni hii.

“Wapo viongozi ambao unawagusa moja kwa moja kama Waziri wa Miundombinu, Bw. Andrew Chenge, ambaye muda wote ana kazi ya kuwatetea Wahindi, hivyo anajua alichokifanya,” alisema mfanyakazi ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Wakati Waziri Mkuu akizungumzia suala la mkataba, wafanyakazi walisema kuwa suala hilo ahojiwe Bw. Chenge ambaye kwa mujibu wa madai yao, ndiye anafahamu kila kitu.

Naye Katibu wa TRAWU, Bw. Sylvester Rwegasira, aliishukuru Serikali kwa uamuzi wake na kuahidi kufanya kazi kwa nidhamu kubwa, ikiwa ni pamoja na kufikisha ujumbe mikoani kote, ili kuachana na mgomo uliokuwapo na safari kwa treni ya abiria kuanza kesho.

“Tumuunge mkono Waziri Mkuu na tuanze kazi mara moja. Tatizo letu
limeondoka sasa tuchape kazi. Nidhamu iwepo na bidii iwepo. Tuna
uhakika Serikali inatujali, inatuangalia,” alisema.

Shirika la RITES la India lilikabidhiwa reli ya kati kuiendesha kwa
ukodishaji kwa miaka 25 kuanzia Oktoba mosi mwaka jana na ikaundwa kampuni ya TRL kufanya kazi hiyo. Serikali ya Tanzania ina hisa 49 na RITES ina hisa 51 katika TRL.

Reli ya kati yenye jumla ya kilometa 2,700 na iliyojengwa zaidi ya
miaka 100 iliyopita, ndiyo njia kuu ya usafiri na uchukuzi nchini kati
ya upande wa Pwani na Bara na hali yake ilikuwa taabani chini ya
Shirika la Reli Tanzania (TRC) ambalo ni la umma na sasa limevunjwa. Mali za TRC ziko chini ya kampuni mpya ya umma ya RAHCO.


 


Source: Majira

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents