Siasa

Pinda: Hatima ya Richmond yaja

WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, amesema ripoti ya kamati teule ya Bunge kuhusu mkataba wa ununuzi wa umeme wa dharura wa Kampuni ya Richmond inatarajiwa kukabidhiwa Machi 26, mwaka huu.

na Salehe Mohamed na Kulwa Karedia

 

 

 

WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, amesema ripoti ya kamati teule ya Bunge kuhusu mkataba wa ununuzi wa umeme wa dharura wa Kampuni ya Richmond inatarajiwa kukabidhiwa Machi 26, mwaka huu.

 

 

 

Alisema hayo jana alipokuwa akifungua semina ya wabunge kuhusu muswada wa sheria ya umeme na biashara ya mafuta, inayotarajiwa kuwasilishwa bungeni kwa ajili ya kujadiliwa katika mkutano wa 11.

 

 

 

Alisema ripoti hiyo ilitoa mapendekezo 23 ambayo serikali iliahidi kuyafanyia kazi na iliamua kuunda timu ya wajumbe kutoka wizara nane chini ya mwenyekiti ambaye alitoka katika tume ya maadili.

 

 

 

Alisema baada ya kukabidhiwa ripoti hiyo ataipitia kwa makini na kisha kuiwasilisha kwa Rais Jakaya Kikwete kwa ajili kuchukuliwa hatua kulingana na maelekezo.

 

 

 

Aidha, alisema ana imani kazi hiyo itakamilika mapema na wabunge na umma utaarifiwa kuhusu hatua zitakazochukuliwa baada ya zoezi la utekelezaji wa mapendekezo litakapokamilika.

 

 

 

“Ninatarajia kuipokea ripoti hii wiki ijayo na nitaipitia kwa makini kisha nitaiwasilisha kwa Rais Kikwete kwa ajili ya maelekezo zaidi, lakini nina imani kazi hii haitachukua muda mrefu,” alisema Pinda.

 

 

 

Kamati hiyo ya Bunge ya kuchunguza mkataba huo iliyoongozwa na Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe, ilimhusisha aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, katika kashfa ya ufisadi kwenye mkataba huo uliolisababishia taifa hasara ya sh bilioni 172.9.

 

 

 

Kutokana na mkataba huo, taifa linaendelea kupata hasara ya sh milioni 152 kila siku kwa kuilipa Kampuni ya Dowans Holdings iliyorithi mkataba huo, mapema mwaka jana.

 

 

 

Kutokana na hayo, Februari 7 mwaka huu, Lowassa alitangaza kujiuzulu wadhifa wa uwaziri mkuu.

 

 

 

Wengine waliojiuzulu kutokana na kashfa hiyo ni aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi na aliyekuwa Waziri wa Afrika Mashariki, Dk. Ibrahim Msabaha, ambaye awali alikuwa akiongoza Wizara ya Nishati na Madini kabla ya kuhamishiwa Afrika Mashariki.

 

 

 

 

 

Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents