Shinda na SIM Account

Polisi 2 wafukuzwa kazi kwa kumpiga mwanasheria

JESHI la Polisi nchini limewafukuza kazi askari wake wawili kutokana na tuhuma za kumpiga Mwanasheria wa Serikali na kumsababishia majeraha mwilini.

Na Chuma Shomari, Tabora


JESHI la Polisi nchini limewafukuza kazi askari wake wawili kutokana na tuhuma za kumpiga Mwanasheria wa Serikali na kumsababishia majeraha mwilini.


Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora, Bw. Daudi Siasi, alisema jana kuwa askari hao Very Joachim na Koplo Ojuku Emmanuel walikuwa wakifanya kazi katika kituo kikuu cha Polisi cha wilaya ya Nzega.


Wakati Bw. Joachim ni askari wa upelelezi Koplo Ojuku ni askari wa kawaida wa jeshi hilo na wamekuwa wakifanyakazi kituoni hapo kwa miaka kadhaa sasa.


Kamanda alisema askari hao walifukuzwa kazi juzi, baada ya Mahakama ya kijeshi kusikiliza mashitaka dhidi yao na kuwakuta na hatia ya kumpiga Mwanasheria wa serikali, Bw. David Zacharia, bila sababu za msingi.


Alisema askari hao walikabiliwa na tuhuma za kumpiga mwanasheria huyo aliyekuwa akifanyia kazi Tabora,akihudhuria kikao cha Mahakama Kuu ya Tanzania mjini Nzega.


Baada ya tukio hilo, Mahakama ilisikiliza mashitaka dhidi ya askari hao na kuwakuta na hatia na kuamuru wafukuzwe kazi na wafikishwe katika Mahakama uraiani kwa ajili ya kukabiliwa na mashitaka zaidi.


Alisema Jeshi la Polisi limetoa adhabu hiyo kwa askari hao liwe fundisho kwa askari wengine wanaotenda kazi zao kinyume cha taratibu na sheria za Polisi na kusababisha madhara kwa wananchi.


Alisema Jeshi hilo liko kwenye zama za kisayansi na kwamba utendaji kazi wake unahitaji nidhamu na uwajibikaji wa uaminifu zaidi na si kuwa na askari wasioheshimu jamii na kufanya kazi kwa pupa na papara ambazo zinasababisha Jeshi kupata lawama lisizostahili.


Askari hao kwa pamoja, walimvamia Mwanasheria huyo Septemba saba mwaka huu, baada ya kumtuhumu kuhusika katika tukio la wizi, katika nyumba ya kulala wageni na kumshambulia kwa kipigo kikali na kumjeruhi.


Kitendo hicho kilisababisha kikao cha Mahakama Kuu Kanda ya Magharibi kilichokuwa kikifanyika Nzega, kuahirishwa baada ya mawakili kuwasilisha hoja, kwamba hawawezi kuendelea na kikao katika mji huo ambao hauna usalama wa kutosha kwani askari wanapiga wanasheria.


Source: Majira

Related Articles

Bongo5

FREE
VIEW