Habari

Polisi adhibiti jambazi mwenye bastola kwa jiwe

ASKARI wa Jeshi la Polisi mjini hapa, amezima jaribio la wizi wa kutumia silaha lililofanywa na majambazi wawili wenye bastola, baada ya kupambana na majambazi hao kwa mawe.

Na Magesa Magesa, Arusha

 

ASKARI wa Jeshi la Polisi mjini hapa, amezima jaribio la wizi wa kutumia silaha lililofanywa na majambazi wawili wenye bastola, baada ya kupambana na majambazi hao kwa mawe.

 

Tukio hilo lilitokea juzi saa 2.30 usiku katika eneo la Chini ya Mti (Idara ya Maji) mjini hapa, baada ya majambazi hao kumvamia Bw. Hebert Mrema (29), anayemiliki duka la kuuza bidhaa za rejareja la H. H. Mrema alipokuwa akijiandaa kufunga.

 

Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Bw. Basilio Matei jana alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa majambazi hao walipofika dukani hapo, walifyatua risasi moja juu kwa lengo la kutawanya watu katika eneo hilo na kutaka kumpiga mmiliki wa duka hilo.

 

Alisema wakati risasi hiyo inafyatuliwa askari alikuwa kwenye daladala akielekea kazini na aliposikia mlio aliamuru gari lisimame ili kujua risasi hiyo inapigwa wapi na kwa nini.

 

Kamanda aliendelea kusema baada ya polisi huyo ambaye alikuwa hana silaha mwenye namba F 4475 Konstebo Patroba, kushuka, aliwaona majambazi hao wakitaka kupora na alipokaribia eneo la tukio mmoja wao alimwelekezea bastola akimwamuru asisogee kwani atamwua.

 

“Kwa ujasiri mkubwa alionao askari huyo, alimfuata na alichukua jiwe kubwa na kumpiga nalo jambazi huyo na kuanguka chini na mwenzake kuona hivyo, alitimua mbio na baada ya wananchi waliokuwa eneo la jirani kuona hali hiyo, walisogea na kutaka kumuua jambazi huyo, ila askari aliwaamuru wasimwue na alikamatwa na kumleta hapa Polisi pamoja na bastola yake,” alisema Kamanda.

 

Alimtaja jambazi huyo aliyekamatwa baada ya kupigwa jiwe na polisi kuwa ni Bw. Joseph Mdoe (28) mkazi wa Ngarenaro mjini hapa na alidai kuwa huwa anajishughulisha na biashara ya mitumba na kwamba mwenzake ambaye bado jina lake halijafahamika, amekimbia na anatafutwa na Polisi.

 

Alisema polisi wanaendelea kumhoji jambazi huyo aliyekutwa na bastola aina ya Revolver B namba 29742 iliyotengenezwa Ufaransa na kwamba atafikishwa mahakamani.

 

Hivi sasa katika mkoa huu, kumeibuka vitendo vya kihalifu hali inayowafanya wakazi mkoani hapa kuishi kwa wasiwasi kutokana na kukithiri kwa vitendo hivyo.

 

Wananchi waliliomba Jeshi la Polisi kuongeza nguvu katika kukabiliana na vitendo hivyo, ambavyo vimeonekana kuibuka kwa kasi ya ajabu mkoani hapa.

 

Source: Majira

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents