Habari

Polisi auawa chumbani kwa hawara

Askari mmoja wa Jeshi la Polisi mkoani hapa, mwenye namba D2600, Konstebo Benny Mwaisamila, ameuawa kinyama kwa kukatwa na shoka kichwani, akiwa chumbani kwa mpenzi wake, aliyetajwa kwa jina la Bi. Mariam Shida (19).

Na Selina Ilunga, PST, Iringa.



Askari mmoja wa Jeshi la Polisi mkoani hapa, mwenye namba D2600, Konstebo Benny Mwaisamila, ameuawa kinyama kwa kukatwa na shoka kichwani, akiwa chumbani kwa mpenzi wake, aliyetajwa kwa jina la Bi. Mariam Shida (19).


Tayari jeshi hilo limesema linamsaka mtu aliyefahamika kwa jina la Juma Richard Ngosha (25), kuwa ndiye anahusika na mauaji hayo.


Habari ambazo zilithibitishwa jana na Kamanda wa Polisi Mkoani Iringa, Bw. Advocate Nyombi, zilieleza kuwa askari huyo alikuwa katika kituo cha kazi cha Ilula, wilaya ya Kilolo mkoani hapa.


Alisema aliuawa usiku wa kuamkia Juni 16, mwaka huu, akiwa kwa mpenzi wake, Bi. Mariam Shida (19) katika eneo la Ilula Mtua `A`.


Imeelezwa kuwa, mtuhumiwa Ngosha alivunja mlango wa chumba ambacho binti huyo amepanga na kuingia ndani kisha kumkata kichwani kwa shoka askari huyo na kutokomea kusikojulikana.


Kamanda Nyombi alikanusha madai kuwa askari huyo alifumaniwa na kusisitiza kuwa askari huyo alikuwa kwa mpenzi wake ambaye hana mume na kwamba marehemu naye hakuwa na mke.


“Bado hatujamkamata mtuhumiwa kwa hiyo hatuwezi kujua kwa nini amefanya mauaji hayo,“ alisema baada ya kuulizwa kama mtuhumiwa alikuwa pia na uhusiano wa kimapenzi na msichana huyo.


Alisema askari huyo alikuwa anatarajiwa kusafirishwa jana kupelekwa kwao mkoani Mbeya kwa shughuli za mazishi.


Aidha, alisema uchunguzi unaendelea na jitihada za kumsaka mtuhumiwa pia zinaendelea.
Hata hivyo, baadhi ya mjirani wamedai kuwa Mariam anayeishi nyumba moja na mtuhumiwa walikuwa wapenzi kabla ya penzi lao kufa hivi karibuni.


Wamedai kuwa Ngosha alifanya mauaji hayo baada ya kuona askari huyo ameingia chumbani kwa mpenzi wake huyo wa zamani na kwamba chumbani kwake alikuwa na mwanamke mwingine.


“Alimtoroka huyo mwanamke na kwenda chumbani kwa Mariam ambako alivunja mlango kwa shoka ambalo pia alilitumia kumuulia marehemu,“ alisema jirani mmoja bila kutaja jina lake.


Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents