Habari

Polisi kuongezwa ili kulinda maalbino

SERIKALI imesema inaangalia uwezekano wa kuongeza askari Polisi mkoani hapa ili kukabiliana na mauaji ya vikongwe na maalbino ambayo yameongezeka siku za karibuni.

Na Wilhelm Mulinda, Mwanza

 

 

 

SERIKALI imesema inaangalia uwezekano wa kuongeza askari Polisi mkoani hapa ili kukabiliana na mauaji ya vikongwe na maalbino ambayo yameongezeka siku za karibuni.

 

Hayo yalisemwa juzi na Waziri wa Mambo ya Ndani, Bw. Lawrence Masha, wakati akihutubia mkutano wa hadhara katika kata ya Isamilo jijini hapa.

 

“Ipo haja ya kuongeza askari Polisi katika mkoa wa Mwanza kwa sababu ya kukabiliana na vitendo vya mauaji ya vikongwe na maalbino ambayo ni tishio kwa maisha ya makundi hayo ya wananchi,” alisema Bw. Masha.

 

Bw. Masha aliwaomba wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi kuwafichua wanaoendesha mauaji hayo na vitendo vingine vya uhalifu ili kuimarisha usalama katika maeneo yao.

 

“Tatizo ni kwamba watu wanaweza kuona uhalifu unatokea sehemu fulani, lakini wanakaa kimya bila kutoa taarifa hizo kwa vyombo vya Dola kwa kuwataja wahusika, sasa uhalifu utakwisha vipi?”, alihoji Bw. Masha.

 

Alisema wananchi wana nafasi kubwa katika kusaidia kudhibiti uhalifu endapo watakuwa tayari kushirikiana na Polisi kwa kutoa taarifa juu ya matukio hayo ikiwa ni pamoja na kuwataja wahusika.

 

Alifafanua, kuwa kwa vyovyote vile wananchi wanawafahamu majambazi, wanaoendesha mauaji ya vikongwe na maalbino kwa hiyo wakitoa taarifa, vitendo hivyo viovu vitakomeshwa katika jamii.

 

Bw. Masha alisema kwa sasa takwimu zilizopo, mkoa wa Mwanza ndio unaoongoza kwa mauaji ya maalbino nchini, kitendo ambacho alidai kinaleta aibu katika mkoa huo.

 

Bw. Masha alikuwa jijini hapa akitembelea jimbo lake la uchaguzi ambapo alifanya mikutano miwili katika kata za Pamba na Isamilo.

 

Naye Subira Mtandi anaripoti kutoka Morogoro, kwamba Mkuu wa wilaya ya Morogoro, Bw. Said Mwambungu, ametaka waganga wa kienyeji wanaopiga ramli na kushawishi watu kutafuta viungo vya binadamu kwa ajli ya dawa kuchukuliwa hatua kali ili kuepuka mauaji ya watu mbalimbali wakiwamo albino.

 

Mwito huo ulitolewa mwishoni mwa wiki iliyopita na Bw. Mwambungu wakati akifungua mkutano wa siku moja wa Chama cha Maalbino Mkoa wa Morogoro.

 

Katika mkutano huo ambao ulikuwa na lengo la kuzungumzia mikakati ya kudhibiti na kupambana na mauaji ya maalbino yanayoendelea katika baadhi ya mikoa nchini, Mkuu wa Wilaya alisema ni lazima Serikali ya mkoa na manispaa, wafanye jitihada za kudhibiti waganga ambao ni chanzo cha mauaji hayo.

 

Alisema kutokana na waganga hao kudanganya watu kuwa viungo vya binadamu hasa maalbino vinaweza kuwafanya wafanikiwe katika shughuli zao ndio maana mauaji ya albino yamekuwa yakiendelea katika mikoa hiyo.

 

Hata hivyo Bw. Mwambungu alisema katika wilaya ya Morogoro vitendo vya mauaji ya maalbino havijatokea na kuahidi kuwa havitatokea, kwani tayari uongozi wa wilaya kuanzia ngazi ya mtaa, umeshaandaa mikakati ya kudhibiti mauaji hayo.

 

Nako mkoani Mbeya, maalbino wametakiwa kuchukua tahadhari kwa kutoa taarifa kwa uongozi wa Polisi na viongozi wa Serikali endapo watakuwa na wasiwasi na watu wanaotaka kuwadhuru.

 

Kauli hiyo ilitolewa jana na Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Bw. Suleiman Kova, alipokuwa akizungumzia mauaji ya maalbino ambayo yamekuwa yakitokea katika mikoa mbali mbali nchini.

 

Kamanda Kova aliwataka maalbino wote kuwa makini katika kipindi hiki na wasitembee peke yao.

 

Alisema maalbino nao wanatakiwa kuwa na uwezo wao wa kujikinga na kuchukua tahadhari katika matukio hayo na si kutembea kwa kujiamini nyakati zote na kuchunga mienendo yao mpaka hapo mauaji hayo yatakapokwisha.

 

Alizitaka kamati za ulinzi na usalama na halmashauri za miji, kusaidia kutatua tatizo hilo kupitia madiwani na watendaji ambao watakuwa na ushawishi mkubwa katika maeneo wanayoishi kupitia mikutano ya hadhara na ya maendeleo na vipeperushi.

 

Pia Kamanda Kova aliwataka waganga wasio rasmi ambao kwa kawaida hupiga ramli wafichuliwe na orodha yao ipatikane kwani ndio chanzo cha mauaji ya maalbino, wazee, watoto na walemavu na kuchukuliwa hatua za kisheria.

 

 

 

Source: Majira

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents