Habari

Polisi kuwasindikiza raia wanaokwenda benki kuwalinda wasiporwe

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limesema kuwa wapo baadhi ya wafanyakazi wa benki, ambao kwa namna moja au nyingine, wanashirikiana na majambazi kufanya uhalifu; na sasa linawasiliana na wamiliki wa taasisi za kifedha, kujiridhisha uhusika wao na uhalifu wa kutumia silaha.

DSC_0345

Aidha, limesema mtu yeyote atakayetaka kusindikizwa na polisi kwenda kuchukua fedha nyingi benki, anaruhusiwa kwa kulipia shilingi 10,000 au Sh 20,000.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi Kanda hiyo, Simon Sirro alisema wameanza kuweka ulinzi mkali katika benki mbalimbali, ikiwemo zilizopo eneo la Mlimani City na kwamba wanakagua pikipiki na watu wanaowatilia shaka.

Kamanda Sirro alisema wapo baadhi ya wafanyakazi wa benki, ambao kwa namna moja ama nyingine wanashirikiana na majambazi kufanya uhalifu, na kutokana na hilo, watawahoji wafanyakazi wa taasisi hizo za fedha ili kubaini ni nani wanaohusika katika njama hizo.

Alisema hiyo ni oparesheni maalumu iliyoanza rasmi na kwamba, uhalifu wa kutumia silaha unaoendelea katika maeneo mbalimbali ya jiji, unahatarisha maisha ya wakazi hao na unapaswa kudhibitiwa haraka. Alisema wananchi wanapaswa kutumia njia mbadala ya kuchukua fedha benki ili kuepuka uhalifu huo.

Alisisitiza kuwa unyang’anyi huo, hufanyika kwa kutumia pikipiki maarufu kama bodaboda na kwamba wameanza oparesheni ya kuwakamata wenye bodaboda hizo na kuwahoji.

“Tumeanzisha oparesheni maalumu dhidi ya pikipiki ambao wanavunja sheria barabarani na wanaojihusisha na masuala ya uhalifu jijini,’’ alisema Kamanda Sirro ambaye ameshika wadhifa huo kuanzia Januari mosi mwaka huu.

Hatua hiyo imekuja baada ya kuripotiwa kutokea kwa matukio kadhaa ya uhalifu, ambapo baadhi ya wananchi ambao ni wateja wa benki wameporwa fedha zao mara tu baada ya kutoka kuchukua katika benki. Baadhi ya benki zinazohusishwa na zile zilizopo katika eneo la Mlimani City katika Manispaa ya Kinondoni.

Source: Habari Leo

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents