Habari

Polisi matatani

NDUGU wa mmiliki wa baa ya Serengeti iliyopo Kihonda mjini Morogoro, Gabriel Assenga (34) aliyeuawa kwa risasi Ijumaa iliyopita, wamedai polisi wanahusika katika mauaji hayo.

NA LEON BAHATI


NDUGU wa mmiliki wa baa ya Serengeti iliyopo Kihonda mjini Morogoro, Gabriel Assenga (34) aliyeuawa kwa risasi Ijumaa iliyopita, wamedai polisi wanahusika katika mauaji hayo.
Wakizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu, ndugu hao walidai mazingira ya tukio yanaonyesha kuwa polisi walihusika, lakini wakajenga mazingira yatakayoonyesha aliuawa na mlinzi wake kwa bahati mbaya.
Baba mdogo wa marehemu, Gasper Assenga alisema Ijumaa iliyopita saa 1:15 jioni marehemu alipata taarifa ya kuwepo vijana wanaohusika na bishara ya dawa za kulevywa katika baa yake, hivyo akaamua kuwapigia simu polisi.
“Kutokana na mazingira ya wasiwasi, alikusanya mauzo na kuingia ndani ya nyumba yake kupumzika,” alisema.
Aliendelea kusema kuwa wakati akiwa ndani, alimtuma mtoto wake kwenda kumnunulia supu na aliporejea aliingia ndani na kufunga geti na wakati huo polisi watatu walifika eneo hilo na kutaka kumuona.
Gasper alisema polisi waliamuru geti lifunguliwe ili waingie ndani, lakini mtoto huyo alipoenda kuomba ridhaa ya baba yake alimkatalia hivyo wakaamua kuingia kwa kuruka wigo wa ukuta.
Alidai polisi hao waliingia ndani na kuanza kuwapiga watoto wakitaka wawaonyeshe aliko baba yao na baada ya muda marehemu alijitokeza na kutaka kufahamu kisa cha kufanya vurugu hizo hasa ikizingatiwa kuwa askari hao aliwafahamu.
“Askari hao alikuwa anawafahamu kwa sababu mara kwa mara walikuwa wakifika kwenye baa hiyo na kunywa naye,” alisema Gasper.
Kwa kuwa alijitokeza akiwa na bastola, Gasper alisema polisi walimvamia kutaka kumnyang’anya na katika vurumai hiyo, marehemu alipiga risasi moja hewani na nyingine kuelekea kwenye geti, wakakimbia wote.
Aliendelea kufafanua kuwa, Gabriel alipata wasiwasi juu ya tukio hilo hivyo akaamua kutoroka kwa kuruka ukuta wa nyumba yake ndipo akajikuta anapigwa risasi akiwa nje.
Familia na majirani walipotoka nje walikuta Gabriel akiwa amekwisha kufa huku mlinzi wa nyumba hiyo akiwa ametoweka.
Usiku huo waliupeleka mwili wa marehemu kuhifadhiwa katika hospitali ya mkoa wa Morogoro na cha ajabu, baba mdogo huyo anadai juzi polisi walienda kuufanyia uchunguzi mwili wa marehemu ‘kinyemela’ wakati ndugu walitaka ufanyike leo ili waliokuwa safarini wawe wamewasili.
“Tukio hilo limetufanya tuamini kuwa polisi wanahusika na walifanya hivyo kutafuta namna ya kupoteza ushahidi,” alisema Gasper.
Ndugu pia walielezea kushangazwa na kitendo cha polisi kutoaa taarifa kwenye vyombo vya habari kuwa aliuawa na mlinzi wake wakati uchunguzi ulikuwa haujafanyika.
Akizungumza kwa simu, baba mkubwa wa marehemu, Baltazar Assenga alisema walienda kulalamika kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Said Kalembo na baada ya kujadiliana na Mkuu wa Wilaya Said Mwambungu na Kamanda wa Polisi wa Mkoa, waliamua gwaride la kuwatambua polisi waliohusika lifanyike jana alasiri.
Naye Kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro, Thobias Andengenye akizungumza na Mwandishi Wetu Latifa Ganzel mjini Mogorogo alisema polisi inaamini mfanyabishara huyo aliuawa na mlinzi wake kwa kudhaniwa jambazi.
Alisema kabla ya kuuawa, mfanyabishara huyo alipiga simu polisi kutoa taarifa kwamba amevamiwa na majambazi na walipofika eneo la tukio hawakukuta kitu hivyo kuamua kuondoka.
Andengenye alisema baadaye mfanyabiashara huyo alipiga tena simu polisi kutoa taarifa ya kuvamiwa na majambazi ambapo polisi walipofika walikuta kuko kimya na kuamua kuingia ndani kwa kuruka ukuta.
Alisema polisi walipoingia ndani mfanyabiashara huyo alitoka akiwa na bastola na alipiga risasi tatu hewani na baadaye kuruka ukuta kutaka kukimbia ndipo mlinzi wake alipompiga risasi akidhani jambazi.
Polisi wanamshikilia mlinzi John Mloka (59) mkazi wa Kilakala ambaye anatoka kampuni ya ulinzi ya Komesha.


Source: Uhuru

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents