Polisi Na Lawama Za Majambazi

Wakati matukio ya ujambazi yakizidi kutikisa Jiji la Dar es Salaam kila kukicha, polisi inakwepa lawama na sasa inawatupia wananchi mzigo kuwa hawatoi ushirikiano wakati wa matukio hayo.

Wakati matukio ya ujambazi yakizidi kutikisa Jiji la Dar es Salaam kila kukicha, polisi inakwepa lawama na sasa inawatupia wananchi mzigo kuwa hawatoi ushirikiano wakati wa matukio hayo.

Ikiwa ni siku moja baada ya tukio la kuibwa kwa shilingi milioni 200 katika kituo cha mafuta cha Gapco eneo la Magomeni, jana tena watu watatu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wakiwa na silaha wamevamia Kanisa la Christian Mission Fellowship lililopo Sinza, Mugabe jijini Dar es Salaam na kumjeruhi mtu mmoja na kufanikiwa kupora kompyuta mbili ndogo.

Akizungumza na Nipashe, Kaimu Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Evarist Mangalla, alisema watu hao wakiwa na silaha walifika kwenye Kanisa hilo mchana na kumlazimisha Katibu Muhtasi wake awafungulie mlango wa ofisi.

Kamanda Mangalla alisema baada ya Katibu Muhtasi huyo kuwagomea waliamua kuupiga mateke mlango huo hadi ulipofunguka.

Alisema watu hao wakiwa ndani ya ofisi hiyo walifanikiwa kuiba kompyuta mbili ndogo na baada ya kutoka kanisani hapo walianza kujihami kwa kufyatua risasi hewani ambapo moja ilimjeruhi kwenye kidole cha mguu mpitanjia.

Alisema baada ya kufyatua risasi hizo kadhaa hewani, watu hao walitokomea mtaani na kompyuta hizo.

Kaimu Kamanda alisema majeruhi aliyepigwa risasi ya kidole, alikimbizwa Zahanati ya Sinza kwa ajili ya matibabu na anaendelea vizuri.

Katika hatua nyingine, Kamanda Mangalla alisema wakati wa tukio la ujambazi likitokea Magomeni juzi, askari wenye silaha ambao hukaa kwenye makutano ya barabara zote za Jiji la Dar es Salaam kila kwenye taa za kuongoza magari, walikuwa wamepewa kazi nyingine ya kufanya.

Hata hivyo, Kamanda Mangalla alipotakiwa kueleza kazi ambayo waliyokuwa wakiifanya askari hao, alisema sio lazima kila kitu kinachofanywa na polisi waandishi wa habari wakijue.

Hata hivyo, aliishia kusema kwamba askari hao walikuwa kwenye kazi pembeni na eneo lilitokea tukio hilo.

Katika uporaji wa juzi polisi imewatupia lawama wananchi ambao walishuhudia tukio hilo kwa kile ilichodai kuwa hawakutoa ushirikiano.

Aidha, jeshi hilo limesema baada ya kufika eneo la tukio wananchi walioshughudia tukio hilo walikataa kutoa ushirikiano na kusababisha watuhumiwa hao kutokomea na fedha hizo ambapo mpaka sasa hawajapatikana.

Mhasibu wa kituo hicho, Seraphine Madenge (47), alikufa baada ya kupigwa risasi tumboni ambayo iliingia upande wa kushoto na kutokea kulia.

Awali akizungumza na waandishi wa habari jana, Mangalla alisema kumekuwa na tabia ya baadhi ya wananchi pindi tukio linapotokea hutupia lawama kwa Jeshi la Polisi bila ya wao kujiuliza wametoa msaada gani.

Kamanda Mangalla alisema baada ya Polisi kufika eneo la tukio mara baada ya kutokea kwa tukio hilo, wananchi waliokutwa hapo hawakutaka kutaja namba za gari lililotumiwa na majambazi hao.

“Mimi nafikiri wananchi wanatakiwa kushirikiana nasi katika kuhakikisha matukio kama haya ya ujambazi yanapotokea basi wawe mstari wa mbele kusaidia ikiwa ni pamoja na kushika namba za magari yanayotumika ili iwe rahisi kwetu na sio kututupia lawama kwamba tunashindwa kazi,“ alisema Mangalla.

 

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents