Habari

Polisi wagundua mabomu kisiwani

JESHI la Polisi wilayani Ukerewe mkoani Mwanza kwa kushirikiana na Jeshi la Wananchi la Tanzania (JWTZ) wilayani humo, limegundua na kuyaharibu mabomu yanayodaiwa kutelekezwa na watu wasiojulikana katika kisiwa kidogo cha Ghana kilichopo ndani ya Ziwa Victoria.

na Sitta Tumma, Mwanza


JESHI la Polisi wilayani Ukerewe mkoani Mwanza kwa kushirikiana na Jeshi la Wananchi la Tanzania (JWTZ) wilayani humo, limegundua na kuyaharibu mabomu yanayodaiwa kutelekezwa na watu wasiojulikana katika kisiwa kidogo cha Ghana kilichopo ndani ya Ziwa Victoria.


Habari zilizothibitishwa na Jeshi la Polisi wilayani humo, zimeeleza kwamba, mabomu hayo mawili, yaliharibiwa juzi katika kisiwa hicho na hakuna madhara yoyote yaliyotokea wakati wa zoezi hilo.


Habari hizo za kipolisi zimeeleza kuwa, mabomu hayo, yaliyotengenezwa nchini Ujerumani, kila moja lilikuwa na uzito wa gramu 175 na kwamba yaligunduliwa na wananchi yakiwa yametelekezwa katika makazi ya watu.


Hata hivyo, polisi wamesema kwamba hadi sasa hakuna mtu yeyote aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo, na uchunguzi wa kina bado unaendelea.


“Tunafanya uchunguzi wa kina ili kubaini nani aliyeleta na kuyatelekeza mabomu haya katika makazi ya watu kisiwani hapo, na kama atapatikana, sheria itafuata mkondo wake bila kuogopa wala kumuonea aibu mtu huyo,” alisema ofisa mmoja wa Jeshi la Polisi wilayani Ukerewe ambaye hakutaka kutajwa jina lake kwa kuwa si msemaji wa jeshi hilo.


Wakati huo huo, jeshi hilo wilayani humo limeapa kuimarisha zaidi ulinzi na usalama katika visiwa vyote vya Ziwa Victoria, ili kuwawezesha wakazi wa visiwa hivyo kuishi kwa amani, usalama na utulivu.


“Si kwamba ulinzi haupo, sisi kama Jeshi la Polisi tunahitaji msaada mkubwa kutoka kwa wananchi wenyewe kuwafichua watu wenye mienendo mibovu kwa kutupa taarifa, lakini nakuhakikishia kuwa ulinzi upo tena thabiti na tutazidi kuuimarisha,” alisema ofisa huyo mwandamizi.


Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents