Polisi wavunja mtandao wa ujambazi

POLISI Dar es Salaam wamevunja mtandao wa majambazi baada ya kuwakamata watuhumiwa wanane na kuwaua wawili wakati wa sherehe za Mwaka Mpya.

Theopista Nsanzugwanko

 

POLISI Dar es Salaam wamevunja mtandao wa majambazi baada ya kuwakamata watuhumiwa wanane na kuwaua wawili wakati wa sherehe za Mwaka Mpya.

 

Watu hao, wengi wao wanadaiwa kuhusika katika matukio tofauti ya uporaji, kujeruhi na kusababisha vifo, likiwamo la uvamizi katika duka la N.L Shah lililopo Chang’ombe lililosababisha kifo cha Polisi, mwandishi wa habari na wizi wa mamilioni.

 

Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,Alfred Tibaigana, alisema Desemba 31, mwaka jana, polisi walipambana na majambazi lakini waliwazidi nguvu na kuwaua majambazi wawili waliodaiwa kuhusika na wizi katika duka N.L Shah mwanzoni mwa mwezi huo ambako Sh milioni 44 ziliporwa.

 

Alisema polisi walipata taarifa kuwa majambazi hao waliofanya uhalifu katika tukio hilo walikuwa Ubungo Kibangu katika nyumba ya Maimuna Kishori wakijiandaa kufanya uhalifu mkoani Mbeya na kuwasiliana nao kisiri ili wakutane nao eneo la Ubungo Plaza.

 

Tibaigana alisema mwanamke huyo anashikiliwa na polisi baada ya kukutwa na bunduki aina ya SMG namba 6006157, ikiwa na risasi 15 ndani ya mfuko wa Rambo pembeni mwa nyumba yake.

 

Alisema mara baada ya majambazi hao kukutana na polisi kuwataka kujisalimisha ili wahojiwe, waligundua walikuwa wakifuatiliwa na Polisi, hivyo kuanza kuwafyatulia risasi askari na hatimaye kurushiana risasi ambako wawili walijeruhiwa na kudondosha bastola zao.

 

Alisema wakiwa wanakimbizwa hospitali walikufa njiani na baadaye walitambuliwa kwa majina ya Hamisi Kishori aliyekuwa akitumia bastola yenye risasi sita na Mohamed Kazi aliyekuwa na bastola aina ya Tokkariv, iliyofutwa namba ikiwa na risasi tano.

 

Alisema katika ufuatiliaji wa tukio hilo, Polisi waliwakamata watuhumiwa wengine na kuwafikisha mahakamani. Aliwataja kuwa ni Ramadhani Bakari (58) mkazi wa Mbagala Kibondemaji ambaye alikuwa dereva wa teksi iliyowabeba.

 

Wengine ni Thadeo Mathias (33) au Kapinga mkazi wa Mwenge, Ramadhani Salum au Rabi (36), Ibrahim Shaban au Marijani Rama (40) mkazi wa Mburahati na Emmanuel Selasi au Adebayor (31) mkazi wa Makoka.

 

Alisema askari walifanya upekuzi katika chumba cha Hamza Nyangali anayedaiwa kuhusika na tukio hilo ambaye anadaiwa kutorokea maeneo ya Lindi na kupata Sh milioni 2. 9 zinazoaminika kuwa mgawo wake katika fedha zilizoporwa.

 

Tibaigana alisema pia wamefanikiwa kuwakamata wanaotuhumiwa kuhusika katika uporaji wa baa iitwayo Happy iliyopo Mongolandege, na baada ya kuwahoji walikiri kuhusika katika tukio la ujambazi lililotokea katika nyumba ya Gabriel Mzava na kumuua Mac Donald Karume (25).

 

Alisema watuhumiwa Joseph Shaban na Michael Kalinga (28) mkazi wa Gongo la Mboto, pia walisadikiwa kuhusika na tukio la mauaji ya mwandishi wa habari wa Redio Uhuru, Japhet Mangula, yaliyotokea Desemba 19, 2007 katika baa ya Sarafina.

 

Kamishna huyo wa Polisi alisema siku ya Mwaka Mpya polisi waliwakamata watuhumiwa ujambazi wawili katika eneo la Ubungo Kibangu baada ya kuvamia baa iitwayo One K na kupora simu tano na fedha taslimu Sh 400,000.

 

Source: Habari Leo

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents