Habari

Polisi ya Tanzania yakiri wasichana waliokamatwa Afrika Kusini na kilo 150 za ‘Unga’ walipitia uwanja wa ndege wa Julius Nyerere na kukaguliwa mizigo yao

Ni takribani siku sita sasa toka wasichana wawili raia wa Tanzania Agnes Gerald na Melisa Edward kukamatwa katika uwanja wa ndege wa OR Tambo Afrika Kusini wakitokea Tanzania, wakituhumiwa kusafirisha dawa za kulevya aina ya Crystal Methamphetamine yenye thamani ya zaidi ya billion 6 za Tanzania.

Swala linalozua maswali mengi ni jinsi gani wasichana hao waliweza kupita katika uwanja wa ndege Julius Nyerere na karibia kilo 150 za dawa hizo za kulevya, kiasi ambacho Mamlaka ya Mapato ya Afrika Kusini imesema ndio mzigo mkubwa zaidi wa dawa za kulevya kuwahi kukamatwa katika mipaka yote ya nchi hiyo kama mzigo mmoja (kwa lugha nyingine imevunja rekodi).

JK Airport

Idara ya polisi nchini Tanzania imekiri kuwa Agnes na Melisa walipitia katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam, na walisafiri na ndege ya shirika la ndege la South African Airways inayomilikiwa na serikali ya Afrika Kusini.

Kamanda wa Polisi Kitengo cha Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa akiongea na NIPASHE jana (June 10) waliotaka kujua wasichana hao walipitia uwanja gani wa ndege na kama walikaguliwa. Alikiri kuwa wasichana hao walikaguliwa kama abiria wengine, lakini akadai kwamba si jukumu la Jeshi la Polisi kufanya ukaguzi kwenye viwanja vya ndege, na kuongeza kuwa ni jambo la kawaida mtu kukamatwa nchi nyingine na dawa za kulevya wakati katika nchi aliyoanzia safari hajakamatwa kwani inategemea utalaamu wa watu wenyewe wanaokagua.

“Kila mtu anapopita uwanja wa ndege anakaguliwa na kama ana kitu ambacho ni kibaya ndipo anakamatwa, hawa wasichana walikaguliwa maana huwezi kupita uwanja wa ndege bila kukaguliwa,” Alisema.

Kamanda Nzowa aliongeza kuwa watu wa uwanja wa ndege ni lazima wawe na mtu au mkaguzi ambaye ni mtaalamu sana wa kutambua dawa za kulevya kwa kuwa ziko za aina nyingi na mbinu nyingi zinatumika kuzisafirisha.

“Utakumbuka Juni 23 mwaka 2010 nilikamata mabalozi wawili, hawa watu walitoka Brazil wakaenda Afrika Kusini, lakini tukawakamatia hapa Tanzania,” alisema Nzowa

Kamanda Nzowa alisema uchunguzi unaendelea kumbaini mmiliki wa dawa hizo na kuna dalili za kuwabaini wahusika hao.

Aliendelea kusema Dawa hizo zilisafirishwa kama mizigo mingine inayokaa sehemu za mizigo ndani ya ndege kwani uzoefu unaonyesha kwamba kwa namna yoyote ile abiria hawezi kuruhusiwa kwenda kukaa na mzigo wake ndani ya ndege unaofikia kilo 150.

Aliongeza kuwa Katika hali ya kawaida, hata kama wasichana hao wangeamua kugawana dawa hizo kwa usawa, kila mmoja angebeba kilo 75, kiasi ambacho hata hivyo abiria haruhusiwi kupanda nacho kama mzigo wa mkononi, wala mzigo ambao haulipiwi.

Taarifa kuhusiana na kukamatwa kwa wasichana Agnes Gerald (25) na Melisa (24) wakiwa na mzigo mkubwa wa dawa za kulevya wenye thamani ya zaidi ya billion 6 kumezua maswali mengi ikiwa ni pamoja na hofu kubwa kutokana na ongezeko kubwa la watanzania wanaozidi kukamatwa wakitaka kusafirisha au kuingiza dawa hizo nchini.

Hivi karibuni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, katika taarifa yake ilisomwa kwa niaba yake na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, mjini Dodoma, katika maadhimisho ya kitaifa ya ‘Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya Duniani’ alisema tatizo la dawa hizo ni janga la kitaifa hivi sasa nchini.

Alisema kumekuwa na wimbi kubwa la Watanzania wanaojiingiza katika biashara haramu ya dawa za kulevya ndani na nje ya nchi na kwamba, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita Watanzania 240 walikamatwa katika nchi za Brazil, Pakistan na Afrika Kusini, kuharibu taswira ya nchi na kusababisha Watanzania wasio na hatia kupata usumbufu na masharti magumu wanapotaka kusafiri kwenda nchi mbalimbali duniani.

Mwezi huu (July) pekee watanzania watano wamekamatwa wakisafirisha dawa za kulevya zenye thamani ya shilingi billion 9.

Kwa mujibu wa Kamanda Nzowa Agnes Gerald na Melisa Edward wameshafunguliwa mashitaka nchini Afrika Kusini.

SOURCE: NIPASHE

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents