Habari

Popobawa azidiwa kete…sasa choka mbaya!

Ile hofu ya baadhi ya wakazi wa maeneo ya Temeke Jijini kuwa kuna ‘dude’ liitwalo popobawa na ambalo huwaingilia watu kimwili nyakati za usiku huenda ikapotea kama moshi hewani baada ya wajanja kuibuka na dawa kali dhidi ya dude hilo.

Na Mwandishi Wa Alasiri

 

Ile hofu ya baadhi ya wakazi wa maeneo ya Temeke Jijini kuwa kuna ‘dude’ liitwalo popobawa na ambalo huwaingilia watu kimwili nyakati za usiku huenda ikapotea kama moshi hewani baada ya wajanja kuibuka na dawa kali dhidi ya dude hilo.

 

Kwa mujibu wa maelezo ya wajanja hao, ni kwamba hiyo dawa ikitumika, popobawa hukosa nguvu na kulainika kama mlenda huku wakati mwingine, akilazimika kutimua mbio toka kwa mtu ambaye tayari ameitumia.

 

Mmoja wa wajanja hao anayedai kuwa bingwa wa kulikomesha dude hilo na kulifanya liwe choka mbaya kwa kukosa nguvu, ni mnajimu maarufu wa Afrika Mashariki na Kati, Sheikh Yahya Hussein wa pale Mwembechai Jijini.

 

Sheikh Yahya ameiambia Alasiri kwa njia ya simu leo asubuhi kuwa wale wanaojaribu kumzuia popobawa kwa kaptula wanacheza tu na badala yake, watumie dawa hiyo ili popobawa asiwatemebelee na kuwahenyesha kwa ‘rigwaride’ kali nyakati za usiku.

 

Kwa mujibu wa Sheikh Yahya, ukihisi eneo ulipo ni hatari kwa popobawa, fanya yafuatayo: Mosi: Weka mifupa ya samaki (hasa aina ya kingfish) kwenye kizingiti cha mlango wako kila asubuhi na jioni.

 

Pili: Weka damu ya kuku ama rangi nyekundu katika kitambaa cheupe na kukifunga mlangoni.

 

Tatu: Twanga kitunguu swaumu na kufunga katika kitambaa cheusi. Kisha weka vitu hivyo chini ya kitanda ama mlangoni.

 

`Ukiyafanya haya, popobawa hatii mguu kwako… na hata akikujia, ataishia kutapika sana na kuishiwa nguvu kwa sababu yeye hapendi vitu hivyo, hasa harufu ya kitunguu swaumu,` akasema Sheikh Yahya.

 

Simulizi za kucharuka kwa popobawa hivi karibuni zilianzia wilayani Mkuranga mkoani Pwani ambapo madiwani Salum Kuga wa Kata ya Mkuranga na Bi. Ashura Mwago wa Viti Maalum waliwahi kukiri kuwa dubwana hilo linawasumbua wakazi wa huko.

 

Pia uvumi huo ukahamia Mbagala, Yombo Dovya na maeneo mengine kadhaa wilayani Temeke.

 

Source: Alasiri

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents