Habari

Radio 5 yafungiwa kwa miezi 3, Magic FM yarudishwa hewani

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imekifungia kituo cha Radio 5 cha mjini Arusha kinachomilikiwa na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kwa kipindi cha miezi 3 pamoja na kuitoza faini ya shilingi milioni 5 huku kituo cha redio cha Magic FM, kikipewa onyo kali pamoja na kutakiwa kuomba radhi kwa muda wa siku tatu mfululizo kwenye vipindi vyao vya taarifa za habari.

radio

Kwa mujiwa wa taarifa iliyosomwa na makamu mwenyekiti wa kamati ya maudhui ya mamlaka hiyo, Joseph Mapunda, TCRA imetoa adhabu hizo kwa kituo cha Radio 5 kutokana na kukiuka baadhi ya Kanuni za Huduma za Utangazaji (maudhui) kupitia kipindi chake cha ‘Matukio’ kilichorushwa Agosti 25, 2016.

“Maneno ya Lema yalilenga kuhamasisha wananchi kupambana na jeshi la polisi na hivyo kusababisha uvunjifu wa amani na kuhatarisha usalama wa taifa,” alisema Mapunda.

“Baada ya kusikiliza maelezo ya utetezi kamati imeridhia kuwa kipindi cha matukio kilikiuka baadhi ya kanuni za maudhui namba 5(a,b,c,d,f,h) 6(2) (b, c) na 18 (1) (b),” ameongeza.

Makamu huyo ameendelea kwa kusema kuwa adhabu hiyo ya faini iliyotolewa kwa kituo hicho cha redio inatakiwa kulipwa ndani ya siku 30 kuanzia leo lakini pia kama watataka kukata rufaa nafasi hiyo ipo wazi kwa muda wa mwezi mmoja.

Akiongelea kuhusu adhabu waliyoitoa kwa kituo cha redio cha Magic FM, Mapunda alisema, “Baada ya kusikiliza na kutafakari kwa kina maelezo ya utetezi yaliyotolewa na uongozi wa Magic FM, kamati imeridhika kuwa kipindi cha ‘Morning Magic’ kilikiuka baadhi ya kanuni za huduma za utangazaji ya mwaka 2005. Kamati ya maudhui inaamua kutoa onyo kali kwa Magic Radio.”

“Pia wanatakiwa kumuomba radhi Rais John Magufuli, wasikilizaji na wananchi kwa ujumla. Tangazo la kuomba radhi litolewe kwa siku tatu mfululizo katika taarifa za habari za saa 10.00 alasiri, na 3.00 usiku kuanzia tarehe 17,9,2016.”

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents