Habari

Rais aliyepinduliwa madarakani na jeshi nchini Sudan, Omar al-Bashir aswekwa gerezani, sababu zaelezwa

Rais aliyepinduliwa madarakani na jeshi nchini Sudan Omar al-Bashir yupo gerezani baada ya kukamatwa Jumanne usiku. Bashir aling’olewa madarakani wiki iliyopita katika mapinduzi ya kijeshi jijini Khartoum baada ya kuiongoza nchi yake kwa miaka 30.

Mwandishi wa BBC nchini Sudan ameongea na vyanzo ndani ya familia ya Bashir ambao wamethibitisha kuwa kiongozi huyo mwenye miaka 75 amekamatwa na kupelekwa jela.

Shirika la habari la kimataifa la Reuters linaarifu kuwa Bashir anashikiliwa kwenye gereza lenye ulinzi mkali la Kobar mjini Khartoum.

Kwa mujibu wa Reuters, al-Bashir anashikiliwa kwenye chumba cha peke yake gerezani na kuzungukwa na ulinzi mkali.

Kiongozi huyo alikuwa chini ya ulinzi mkali wa jeshi nyumbani kwake toka alipopinduliwa wiki iliyopita.

Luteni Jenerali Abdel Fattah Abdelrahman Burhan
Image captionLuteni Jenerali Abdel Fattah Abdelrahman Burhan ndiye mkuu wa baraza la mpito la kijeshi linaloongoza Sudan

Nchi ya Sudan kwa sasa ipo chini ya uongozi wa Baraza la Mpito la Kijeshi chini ya Luteni Jenerali Abdel Fattah Abdelrahman Burhan.

Katika hotuba kwenye televisheni siku ya Jumamosi, Jenerali Burhan aliapa “kuung’oa utawala”, na kuahidi kuheshimu haki za binaadamu, kusitisha marufuku ya kutotoka nje, kuwaachia huru wafungwa wa kisiasa, kuvunjilia mbali serikali zote za majimbo, kuwashtaki waliowaua waandamanaji na kukabiliana na rushwa.

Baraza hilo limewakamata baadhi ya waliokuwa maafisa wa serikali na kuahidi kutowatawanya waandamanaji.

Msemaji mmoja pia aliuomba upinzani kumchagua waziri mkuu mpya na kuahidi kumuidhinisha watakayemchagua.

Waandamanaji Sudan
Image captionWaandamanaji Sudan wanataka jeshi liachie hatamu za madaraka kwa uongozi wa kiraia

Katika mkutano na waandishi habari siku ya Jumapili, msemaji wa baraza Meja Jenerali Shams Ad-din Shanto ameeleza kwamba baraza la kijeshi lipo “tayari kuidhinisha” serikali yoyote ya kiraia itakayoidhinishwa na vyama vya upinzani.

“Hatutomteua waziri mkuu. Watamchagua,” alisema akimaanisha upinzani na makundi yanayoandamana.

Ameeleza pia kwamba jeshi halitowaondoa waaandamanaji kwa lazima lakini ametoa wito kwa waandamanaji hao “kuruhusu maisha yaendelee kama kawaida” na waache kuweka vizuzi kinyume cha sheria.

“Kushika silaha hakutoruhusiwa,” aliongeza.

‘Uganda kumpa hifadhi al-Bashir’

Bashir alivyong'oka madarakani

Serikali ya Uganda imesema ipo tayari kumpatia hifadhi bwana al-Bashir endapo ataomba kuishi Uganda baada ya kupinduliwa na jeshi.

Waziri wa Mambo nje wa Uganda Henry Okello Oryem ameliambia shirika la habari la AFP kuwa: “Endapo Uganda itaombwa kumpatia hifadhi suala hilo litashughulikiwa katika kiwango cha juu cha uongozi wa nchi yetu.”

Oryem amesema Uganda inatambua na kuheshimu kazi kubwa aliyoifanya katika kuleta amani na kupatikana kwa uhuru wa Sudan Kusini.

“Uganda haitaomba radhi wala kujutia hatua yake ya kuwa tayari kumuhifadhi Bashir,” aliongeza Waziri huyo.

Bashir anatafutwa na Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) kwa tuhuma za kukiuka haki za kibinaadamu na uhalifu wa kivita kwenye mgogoro jimboni Darfur.

Ikiwa kama mwanachama wa Mkataba wa Roma ambao ulianzisha mahakama ya ICC, Uganda watakuwa kwenye shinikizo la kumsalimisha Bashir kwenye mahakama hiyo endapo watampa hifadhi.

By Ally Juma.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents