Habari

Rais Donald Trump amtusi rais wa Ufaransa Macron na kusema ‘Nato ni ubongo uliyokufa’ – Video

Rais Donald Trump amtusi rais wa Ufaransa Macron na kusema 'Nato ni ubongo uliyokufa' - Video

Rais wa Marekani Donald Trump amemkosoa vikali mwenzake wa Ufaransa Emmanuel Macron kwa kusema Nato ni “ubongo uliyokufa” na kuongeza kuwa tamko lake ni ”matusi”. Bwana Trump yuko nchini Uingereza kuhudhuria mkutano wa muungano wa kujihami kwa mataifa ya magharibi, Nato unaoadhimisha miaka 70 tangu ulipobuniwa.

Akiwa katika mkutano na wanahabari, Bwana Trump amesema Nato, inajukumu muhimu na matamshi ya Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ni “matusi”.

Bwana Trump amesema anaona Ufaransa ikijiondoa kutoka kwa Nato, lakini hakuelezea sababu zake.

Nato – muungano wa kujihami kwa mataifa ya magharibi uliundwa baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia kukabaliana na kitisho cha uwezekano wa kuendelea kutanuka kwa muungano wa Usoviet.

Bwana Macron alielezea muungano huo kama “ubongo uliokufa”, akisisitiza kile anachokiona kama kutokuwa na utashi wa mdhamini mkuu wa Marekani.

Mkutano huo unaotajarajiwa kuanza hii leo Jumanne baadaye, tayari umekumbwa na mzozo mkali kati ya wanachama wake Ufaransa na Uturuki, pamoja na muendelezo wa suala la mchango wa mataifa mwanachama.

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, amesema kwamba atapinga mpango wa Nato wa kiulinzi kwa nchi za Baltiki iwapo haitaiunga mkono Uturuki katika vita vyake dhidi ya kikundi cha Kikurdi ambacho inakichukulia kama cha kigaidi.

Trump amesema nini?

Akiwa ameketi karibu na katibu mkuu wa Nato, Jens Stoltenberg, Bwana Trump amesema muungano wa Nato, “una jukumu muhimu”, lakini pia alipoulizwa mtazamo wake kuhusiana na matamshi ya Bwana Macron.

Trump alijibu kuwa kiongozi huo wa Ufaransa, “amezikosea heshima” nchi zengine mataifa wanachama.

“Matamshi yake ni machafu. Nadhani Ufaransa ina kiwango kikubwa cha ukosefu wa kazi. Uchumi wa Ufaransa wenyewe hauko vizuri, “alisema.

“Ni matamshi makali sana kwa mtu kuyazungumza huku Ufaransa ikiwa inapitia kipindi kigumu kama hichi hasa ukizingatia kile kinachoendelea. Mwaka huu wamekuwa na wakati mgumu kweli. Huwezi kuanza kuzunguka huku na kule ukisema matamshi kama haya kuhusu Nato. Huu ni ukesefu heshima wa hali ya juu.”

Bwana Trump ameongeza: “Kwa wakati huu hakuna anayehitaji usaidizi wa Nato kama Ufaransa… Manufaa inayopata Marekani ni machache mno. Huu ni usemi hatari sana. “Ninamwangalia [Bwana Macron] kisha najiambia, anahitaji ulinzi zaidi ya mwengine yoyote hivi sasa lakini pia namuona akijiondoa kutoka kwa Nato. Hata hivyo ni jambo ambalo halijanishangaza kwa kweli.”

Vilevile, Bwana Trump amerejelelea malalamishi yake ya muda mrefu kwamba mataifa mengine wanachama wa muungano wa Nato, hawachangii kama inavyohitajika kipesa na kuitaja Ujerumani kama mfano.

Bendera ya NATOHaki miliki ya pichaREUTERS
Image captionBendera ya NATO

Mataifa wanachama wa Muungano huo 29 waliahidi kusaidiana iwapo mmoja wao atashambuliwa.

Lakini kulingana na mazungumzo ya Bwana Macron mwezi uliopita, alilalamikia ukosefu wa wanachama wa Nato kwamba hawatoi tena ushirikiano katika masuala muhimu.

Mwezi uliopita, rais wa Ufaransa aliitaja Nato kuwa muungano ”usio na maana”, akisema kuwa wanachama wake hawashirikiani kuhusu masuala muhimu.

Rais wa Marekani Donald Trump ni miongoni mwa viongozi watakaohudhuria mkutano huo.

Aliwasili nchini Uingereza siku ya Jumatatu kabla ya hafla maalum itakayoandaliwa na malkia katika kasri la Buckingham Palace Jumanne jioni.

Bwana Trump pia anajiandaa kufanya mazungumzo ya pembeni na viongozi wa Ujerumani, Ufaransa na katibu mkuu wa Nato.

Hali ya taharuki imekuwa ikipanda tangu rais Trump, alipolalamika mara kadhaa kuwa mchango wa mataifa ya Ulaya ambayo ni wanachama wa Nato haukidhi mahitaji ya shirika hilo ambalo lilibuniwa kukabiliana na vitisho baada ya vita vikuu vya pili vya dunia ili kupanuka kwa ukomyunisti baada ya vita vya pili vya dunia.

Mkutano huo unafanyika wakati ambapo rais Trump anakabiliwa na uchunguzi kuhusu tuhuma dhidi yake huku akijiandaa kwa kampeini ya uchaguzi mwaka ujao.

Huku hayo yakijiri Uingereza inaelekea kufanya uchaguzi mkuu wiki ijayo licha ya mchakato wa nchi hiyo kujiondoa kutoka muungano wa ulaya maarufu Brexit.

Wanachama wa Nato wameahidi kusaidiana endapo moja kati ya washirika wake 29 atashambuliwa.

Kabla ya ziara yake, rais Trump aliandika katika Twitter kujipongeza kuhusu tamko la hivi karibuni la katibu mkuu wa Nato Jens Stoltenberg la kuongeza bajeti.

Nato inakadiria kuwa kufikia mwaka 2019 ni mataifa manane miongoni mwao Marekani ndio yalioafikia viwango vya mchango uliowekwa kama ilivyokubaliwa na mataifa wanachama.

Mataifa hayo yalikubaliana kwamba yatumie 2% au zaidi ya pato la jumla la serikali kwa ulinzi.

Bwana Stoltenberg siku ya Ijumaa alisema kufikia 2020, washirika wa Ulaya na Canada watakuwa wamewekeza dola bilioni 130 sawa na (£100bn) zaidi tangu 2016, mwaka ambao rais Trump alichaguliwa.

Kabla ya mkutano huo, Waziri wa Ulinzi wa Marekani Mark Esper ameitaka Uturuki kutokuwa na msimamo katika suala la mpango wa ulinzi wa Nato kwa nchi za Baltik na Poland katika jaribio lake la kutafuta uungwaji mkono huko kaskazini mwa Syria.

“Umoja katika muungano na utayari, kuna maanisha kuangazia masuala muhimu zaidi…Na siyo kila mmoja yuko tayari kuunga mkono ajenda zake. Siyo kila mmoja anaona vitisho inavyoviona Uturuki, ” ameliambia shirika la habari la Reuters

Lakini akizungumza katika mji wa Ankara kabla ya mkutano huo, Bwana Erdowan amesema Uturuki itapinga mpango huo ikiwa Nato haitatambua kundi wanalopigana nalo kama la kigaidi.

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan (kushoto) na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron Picha ya: Octoba 2018Haki miliki ya pichaAFP/GETTY IMAGES
Image captionJe Bwana Erdogan (kushoto) na Bwana Macron watajaribu kusuluhisha mzozo kati yao?

Masuala mengine ni yapi?

Katika mahojiano mwezi uliopita Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron aliuelezea Muungano wa Nato kama “ubongo” uliokufa, akisisitiza kile anachokiona kama kutokuwa na utashi wa mdhamini mkuu wa Marekani kwa Muungano huo wa kujihami wa nchi za magharibi.

Alitaja hatua ya Marekani kuondoa vikosi vyake kaskazini mwa Syria bila kushauriana na muungano huo mwezi Octoba, na kuipatia nafasi Uturuki kuvamia kijeshi maeneo yanayodhibitiwa na wapiganaji wa Kikurdi ili kubuni “eneo salama” katika mpaka wake.

Hatiua hiyo ya kijeshi ilizorotesha uhusiano kati ya Uturuki na wanachama wengine wa Nato.

Ijumaa iliyopita, Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alijibu tamko la Macron akisema kuwa yeye ndiye “amekufa akili”. Alimkosoa akisema kuwa “ni mgonjwa na mwenye uelewa mdogo” kuhusiana na ugaidi.

Nato ni nini?

  • Muungano wa kujihami wa nchi za magharibi ni muungano wa kiulinzi wa kikanda wenye nguvu zaidi.
  • Ulianzishwa mwaka 1949, baada ya Vita Vikuu Vya Pili vya Dunia, wakati kukiwa na wasiwasi wa kupanuka zaidi kwa Muungano wa Usovieti.
  • Muungano huo uliundwa kwa misingi ya ushirikiano wa kiulinzi kati ya washirika wake ambao awali walikuwa 12 lakini kwa sasa wameongezeka na kufikia 29.

By Ally Juma.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents