Habari

Rais Hussein Mwinyi atoa miezi mitatu kwa uongozi wa Wizara ya Afya Zanzibar (Video)

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ametoa muda wa miezi mitatu kwa uongozi wa Wizara ya Afya kurekebisha kasoro za kiutendaji zinazosababisha kutokuwepo ufanisi katika utoaji wa huduma bora kwa wagonjwa.

Dk. Mwinyi ametoa kauli hiyo wakati alipofanya ziara ya kushtukiza katika Hospitali ya Rufaa ya Mnazi mmoja, alipofika kuangalia utoaji wa huduma kwa wagonjwa katika maeneo na vitengo tofauti vya Hospitali hiyo.

Alisema kwa kiwango kikubwa mambo mengi yanahitaji kufanyiwa marekebisho, akibainisha kuwepo changamoto mbali mbali za kiutendaji na hivyo kuzorotesha uapatikanaji wa huduma bora kwa wagonjwa.

Alisema analenga kuchukua hatua za kiutawala dhidi ya watendaji wasiowajibika kazini na kusababisha wananchi kulalamika kutokana na ukosefu wa huduma, pamoja na kupewa lugha zisizordhisha kutoka kwa wauguzi na watendaji wengine wa Hospitali hiyo.

Aidha, Dk. Mwinyi alisema pamoja na Serikali kuipatia fedha za kutosha Hospitali hiyo kila mwezi, kumekuwepo changamoto za ukosefu wa vifaa muhimu kwa wagonjwa ikiwemo magodoro, dawa na vifaa vya maabara, hivyo akautaka Uongozi wa Hospitali hiyo kubadilika na kuondokana na utendaji wa mazowea.

Alisema pale Serikali inapotoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa dawa na hatimae wagonjwa wakakosa dawa hizo, ni dhahiri kuwa kuna tatizo mahala hapo.

Alieleza kuwa kumekuwepo matatizo madogo madogo katika uendeshaji wa Hospitali hiyo na kubainisha kuwa; kama yangelishuhulikiwa ipasavyo , ni wazi kuwa huduma bora zingepatikana.

Aidha Rais Dk. Mwinyi , aliahidi kufanya ziara nyingine katika siku zijazo na kuzungumza na wafanyakazi kwa lengo la kuimarisha utendaji na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Alisema wafanyakazi wana wajibu wa kuwatumikia wagonjwa kikamilifu sambamba na kupata haki wanazostahili.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents