Siasa

Rais Kikwete amteua Augustino Ramadhan Jaji Mkuu

RAIS Jakaya Kikwete amemteua Jaji Augustino Ramadhan kuwa Jaji Mkuu wa nne wa Tanzania, baada ya Jaji Mkuu Barnabas Samatta kustaafu rasmi.

Jaji Augustino RamadhanNa Mwandishi Wa Mwananchi


RAIS Jakaya Kikwete amemteua Jaji Augustino Ramadhan kuwa Jaji Mkuu wa nne wa Tanzania, baada ya Jaji Mkuu Barnabas Samatta kustaafu rasmi.


Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Phillemon Luhanjo jana, uteuzi wa Jaji Ramadhan ambaye ni Jaji wa Mahakama ya Rufani kwa muda mrefu sasa, unaanza mara moja.


Taarifa hiyo ilielezea kuwa Jaji Ramadhani ataapishwa kesho jioni Ikulu jijini Dar es Salaam.


Jaji Ramadhani ambaye ni mwenye vipaji vingi, kabla ya kuingia katika shughuli za mahakama, alikuwa katika jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) akifanya kazi huko katika Idara ya Sheria na alitoka jeshini akiwa na cheo cha Brigedia Jenerali.


Pia amewahi kuwa Jaji katika Mahakama ya Afrika Mashariki ambako alikuwa yeye pamoja na Waziri Mkuu wa zamani wa Tanzania, Jaji Joseph Warioba, walikuwa wakiiwakilisha Tanzania.


Kwa upande wake, Kenya ilikuwa ikiwakilishwa na Jaji Moijo ole Keiwu na Jaji Kassanga Mulwa walioteuliwa na Rais wa zamani wa Kenya, Daniel arap Moi.


Kwa Uganda walikuwapo majaji Joseph Mulenga na Jaji Solony Bosse, aliyepata kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria wa Afrika Mashariki.


Sambamba na hilo, Jaji Ramadhan pia ni mpiga kinanda maarufu katika kwaya ya wa Kanisa la Anglikana jijini Dar es Salaam.


Taarifa iliyotolewa juzi kwa vyombo vya habari na Idara ya Habari (Maelezo), ilisema kuwa Mahakama ya Tanzania itafanya kikao maalum cha kumuaga kitaaluma Jaji Msataafu Samatta, ambacho kitafanyika Julai 19, mwaka huu kwenye jengo la Mahakama ya Rufani iliyopo Kivukoni Front.


Taarifa hiyo ilieleza kuwa Jaji Samatta atastaafu ifikapo Julai 20, mwaka huu.


Katika shughuli za kumwaga, atakagua gwaride la heshima mbele ya jengo hilo.


Miongoni mwa watu watakaohudhuria siku hiyo ni Waziri Mkuu, Edward Lowassa, Waziri wa Sheria na Katiba, Dk Mary Nagu akiwemo Naibu wake, Mathias Chikawe, na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika ambaye atatoa hotuba.


Mbali na Jaji Samatta, Watanzania wengine wazalendo waliowahi kushikilia nafasi ya Jaji Mkuu ni Augustino Saidi na Francis Nyalali.


Hii ina maana kwamba Jaji Ramadhan anakuwa pia Mzanzibari wa kwanza kushika wadhifa wa juu katika duru za mahakama nchini Tanzania.


Source: Mwananchi

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents