Siasa

Rais Kikwete awabana mawaziri kuhusu ufujaji

RAIS Jakaya Kikwete amewabana mawaziri wake kwa kusema kwamba kuanzia sasa ni wao watakaowajibika kwa matumizi mabaya ya fedha za umma katika wizara wanazoziongoza.

Mwandishi Wa Habari Leo


RAIS Jakaya Kikwete amewabana mawaziri wake kwa kusema kwamba kuanzia sasa ni wao watakaowajibika kwa matumizi mabaya ya fedha za umma katika wizara wanazoziongoza.


Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ikulu, Rais Kikwete alitoa msimamo huo jana mjini Dodoma wakati alipokutana na watendaji wakuu katika Serikali Kuu, Wakuu na Makatibu Tawala wa Mikoa kuijadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Rais Kikwete, ambaye alifanya kikao kama hicho na mawaziri Ijumaa wiki iliyopita alisema; viongozi wa kisiasa kwa maana ya mawaziri na wakuu wa mikoa na wilaya ingawa si watendaji, lakini wanawajibika kwa yanayotokea katika sehemu wanazoziongoza.


“Wewe Waziri ndiye unayewekwa kizimbani pale bungeni, si Katibu Mkuu wala Mhasibu. Hao wanakuwa hawapo … Siku zote unayewajibika ni kiongozi wa kisiasa. Usikubali kufa kibudu,” taarifa kutoka Ikulu imemnukuu Rais akisema.


Aliwatahadharisha wajumbe wa kikao hicho kwamba, fedha zinazotolewa na serikali ni kwa ajili ya maendeleo ambayo yanatakiwa kuonekana.


“Fedha hizi ni za serikali jamani. Haziwezi kuwa kama fedha za ubani, unaotoa kwenye msiba halafu huulizi zimetumikaje. Fedha hizi za serikali lazima tuulizane zimetumikaje na kama zimetumiwa kwa malengo yaliyokusudiwa na matokeo yake lazima yaonekane,” alisema.


Aliwaeleza waliohudhuria kikao hicho kwamba wakati sasa umefika kwa mamlaka zinazohusika kuwawajibisha watendaji ambao hawatekelezi majukumu yao kwa kuzingatia kanuni, sheria na taratibu za kazi zao.


“ Tunatambua kuwa zipo adhabu zilizotamkwa kwa mujibu wa sheria kwa wahusika wasiotimiza wajibu wao. Sasa imefika wakati kwa mamlaka husika kuwawajibisha wasiotimiza wajibu,” alisisitiza Rais. Taarifa imemnukuu Rais akisema kwamba hategemei na wala si matumaini yake kwamba baada ya kikao cha jana ambacho waliohudhuria waliijadili kwa kina taarifa ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali na kuweka mikakati ya kurekebisha kasoro zilizojitokea, kujiwekea malengo ya kutorudia tena makosa hayo, ripoti za miaka ijayo zitakuwa mbaya.


“Kama baada ya kikao hiki, kutatokea mtu yule yule anarudia yale yale, basi au kazi hajui na tutamwambia akatafute kazi nyingine, au anafanya makusudi, lakini kwa yote hayo lazima awajibishwe. Maana hii itakuwa sawa na kutia pamba masikioni,” alisema. Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Makamu wa Rais, Dk Ali Mohammed Shein, Waziri Mkuu Edward Lowassa na Spika wa Bunge, Samuel Sitta.


Ilikubaliwa baada ya kikao cha jana kwamba kuanzia sasa kila mwaka ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali, mara baada ya kuwasilishwa kwake, zitakuwa zinajadiliwa katika ngazi ya Baraza la Mawaziri, ngazi ya mkoa na katika Halmashauri za Miji, na kwamba Madiwani lazima washirikishwe kikamilifu. Kikao cha jana kitafuatiwa na kingine cha Watendaji Wakuu katika Serikali za Mitaa Jumapili Aprili 29, ambacho pia kitakuwa chini ya Rais Kikwete.


Source: Habari Leo

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents