Aisee DSTV!

Rais Magufuli acheza kama Pelé nchini Afrika Kusini, Afungua fursa kwa Walimu wa somo la kiswahili Tanzania

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 26 Mei, 2019 amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini, Mhe. Cyril Ramaphosa, Ikulu Jijini Pretoria.

Rais Magufuli na Ramaphosa

Katika Mazungumzo hayo, Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mhe. Rais Ramaphosa kwa kuapishwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Afrika Kusini na amemhakikishia kuwa Tanzania itadumisha uhusiano na ushirikiano wa kindugu na kihistoria na nchi hiyo ulioasisiwa na Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Hayati Nelson Mandela kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha ANC (African National Congress).

Mhe. Rais Magufuli amemshukuru, Mhe. Rais Ramaphosa kwa kumkaribisha kufanya nae mazungumzo siku moja baada ya kuapishwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Afrika Kusini na amebainisha kuwa anatarajia uhusiano wa Tanzania na Afrika Kusini utaimarishwa zaidi katika masuala ya uchumi na kukuza lugha ya Kiswahili.

Kwa upande wake, Mhe. Rais Ramaphosa amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwake, na amemhakikishia kuwa Afrika Kusini inatambua mchango mkubwa wa Tanzania katika ukombozi wa Taifa hilo na kwamba katika kipindi chake cha uongozi atauendeleza na kuuza zaidi uhusiano huo.

Mhe. Rais Ramaphosa amesema kufuatia uamuzi wa Afrika Kusini kuanza kufundisha lugha ya Kiswahili, nchi yake itachukua walimu wa Kiswahili kutoka Tanzania ili watumike kufundisha somo hilo katika shule za msingi na sekondari.
Aidha, Mhe. Rais Ramaphosa ameahidi kufanya Ziara Rasmi ya Kitaifa nchini Tanzania kabla ya Mkutano wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) uliopangwa kufanyika mwezi Agosti 2019 nchini Tanzania.

Kabla ya mazungumzo hayo Mhe. Rais Magufuli ambaye ameongozana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi amemkabidhi Mhe. Rais Ramaphosa zawadi ya vitabu vya kusoma na kufundishia lugha ya Kiswahili kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Mhe. Rais Magufuli na Mhe. Rais Ramaphosa wamefanya mazungumzo hayo ikiwa ni kabla Mhe. Rais Ramaphosa hajatangaza Baraza lake la Mawaziri.

Related Articles

Back to top button
Bongo5

FREE
VIEW