Burudani

Rais Magufuli afuta tena sherehe za uhuru, aagiza fedha zilizotengwa zitumike kujenga hospitali (+audio)

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameahirisha maadhimisho ya sherehe za Uhuru zilizotarajiwa kufanyika Desemba 9, 2018 na fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya kufanikisha shamra shamra hizo ameelekeza zitumike kujenga hospitali mkoani Dodoma itakayoitwa hospitali ya Uhuru.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana (Novemba 20, 2018) na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Rais Magufuli ameagiza kiasi cha Sh995.18 milioni zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya kufanikisha sherehe hizo zitumike kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo.

Waziri Mkuu ametoa taarifa hiyo wakati alipokutana na viongozi waandamizi wa mkoa wa Lindi pamoja na wilaya zake katika kikao cha maandalizi ya shughuli za kuzima Mwenge kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi.

Hii ni mara ya pili kwa Rais Magufuli kuahirisha sherehe za uhuru, ambapo awali alifanya hivyo Desemba 2015 mwezi mmoja tu tangu aingie madarakani. Fedha zilizotengwa aliagiza zitumike kupanua kipande cha barabara kutoka Morocco hadi Mwenge Jijini Dar es Salaam.

Pia siku hiyo ya Desemba 9, 2015, Rais Magufuli alishiriki kufanya usafi katika maeneo ya kuzunguka Ikulu Jijini Dar es Salaam hadi katika soko la samaki la feri na kueleza kuwa ni aibu kwa Taifa kukumbwa na kipindupindu kwa sababu ya uchafu.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents