Aisee DSTV!
SwahiliFix

Rais Magufuli aitaka Sekretarieti ya SADC kujitathmini, hotuba yake yapokelewa kwa shangwe (+Video)

Mwenyekiti Mpya wa Jumuiya ya maendeleo Kusini mwa Afrika SADC, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Magufuli amezitaka Jumuiya za Kimataifa kuiondolea vikwazo vya kiuchumi nchi ya Zimbabwe.

Rais Magufuli amekabidhiwa Uenyekiti wa nchi za jumuia ya maendeleo kusini mwa Afrika SADC leo kutoka kwa Rais wa Namibia Dk. Hage Geingob alioutumikia wadhfa huo kwa muda wa mwaka mmoja.

Akizungumza mbele ya wakuu wa nchi na viongozi wa Serikali kutoka nchi 16 za jumuiya hiyo Mwenyekiti huyo amesema umefika wakati kwa jumuiya za kimaifa kuiondolea vikwazo Zimbabwe kwani madhara yake si kwa nchi hiyo pekee bali na kwa nchi nyingine za Afrika, “Zimbabwe imewekewa vikwazo vya kiuchumi kwa muda mrefu. Naitolea mwito sasa jumuiya ya kimataifa waiondolee vikwazo hivyo vya kiuchimi.” alisema Rais Magufuli mwanzoni kabisa mwa hotuba yake iliodumu kwa takriban dakika arobaini.

Rais magufuli pia amezitaka nchi zinazounda jumuiya hiyo kuwa na kauli moja katika kukabiliana na changamoto zinazoikumba jumuiya hiyo ikiwemo hali ya umasikini kwa wananchi.

“Haina tofauti na mwili wa binadamu iwapo kiungo kimoja kina tatizo maana yake ni mwili wote hauko sawa” alisisitiza Mwenyekiti huyo mpya wa SADC atakayetumikia nafasi hiyo kwa mwaka mmoja kuanzia leo.

DHANA YA VIWANDA KUIKOMBOA SADC DHIDI YA UMASIKINI

Katika kipindi cha mwaka 2017/2018 pato la ndani katika jumuiya hiyo linatajwa kukua lakini si kwa kiwango cha kuridhisha kama ambavyo wamejiwekea kiwango cha kufikia asilimia saba kwani ni Tanzania pekee inatajwa kufikisha kiwango hicho.

Katibu Mkuu wa SADC Dk.Stergomena Laurance Tax, amesema kuwa nchi zote  zimekuwa zikifanya jitihada za kufikia kiwango hicho lakini hadi sasa ni Tanzania pekee ndio imefikia kigezo hicho ambacho wamejikiwea cha kuwa na uchumi mpana.

Amefafanua iwapo hakutakuwa na jitihada za pamoja ni vigumu kufikia malengo ambayo wamejiwekea, hivyo amewataka viongozi wa jumuiya hiyo kujipanga upya ili kwenda pamoja na kukamilisha miongoni mwa azma ya jumuia ambayo ni ukombozi wa kiuchumi.

Ameuambia mkutano kuwa, mwaka jana SADC ilikuwa imejipangia kuwa na uchumi wa zaidi ya asilimia saba lakini imefikia asilimia 3.1 , hiyo ikiwa ni chini ya asilimia ya umoja wa Afika(AU) iliyofikia asilimia 3.5 na Afrika Mashariki asilimia 5.7 , Afrika Kaskaziniki asilimia 4.8 na Afrika Magharibi asilimia 3.3.

Hata hivyo imeelezwa kuwa moja sababu ya kuendelea kudidimiza uchumi wa jumuia hiyo yenye zaidi ya miongo miwili na nusu ni pamoja na uuzwaji wa malighafi za viwanda nje ya Afrika, hatua iliyopingwa vikali na Mwenyekiti mpya Rais John Magufuli wa Tanzaia ambaye mara zote ameonekana akipigia chepuo uchumi unaojipwekesha  kwenye viwanda.

SEKRETARIETI YA SADC YATAKIWA KUJITATHIMINI

Akimalizia hotuba yake Mwenyekiti wa SADC Rais John Magufuli ameitaka sekretarieti ya jumuiya hiyo kujitathimini kwani bado haijaonesha mchango wake ipasavyo kuzisaidia nchi zinazounda jumuiya kupiga hatua za kiuchumi.

“Nataka tuseme ukweli na hakuna sababu ya kuficha bado sekretarieti ya SADC haijanifurahisha kwani takwimu za kiuchumi zimekuwa zikishuka siku hadi siku  na sekretarieti haina msaada unaotosha. Hii ni changamoto kwenu ninyi na mjitathimini,”amesema Rais Magufuli huku akishangiliwa na mkutano huo uliohudhuriwa na idadi ya watu zaidi ya 1000.

HALI YA KIDEMOKRASIA NA CHANGAMOTO YA KIUSALAMA

Mwenyekiti wa zamani wa jumuiya hiyo ambaye pia ni Rais wa Namibia Dk. Hage Geingob amesema tathimini ambayo wameifanya inaonesha kukua kwa demokrasia hasa kwa kuzingatia nchi za jumuiya hiyo zimekuwa zikifanya chaguzi zake kwa huru na haki na kupata viongozi wake.

Amefafanua kukua kwa demokrasia kumesababisha kwenye mkutano wa 39 wa jumuiya hiyo kuwepo na marais wapya ambao wamepatikana kupitia chaguzi ambazo zimefanyika katika nchi zao akitolea mfano Rais wa Congo DRC, Msumbiji na Zimbabwe.

“Ni jambo la faraja kwa nchi za SADC kuona demokrasia yake inazidi kuimarika siku hadi siku.Nchi zetu zimekuwa zikifanya chaguzi zilizo huru na haki.Kwetu hili ni jambo la kujivunia na kubwa zaidi kuhakikisha tunaendelea kuimarisha demokrasia katika nchi zetu,”amesema Dk. Geingob.

Hata hivyo hali ya kutetereka kwa usalama kwa baadhi ya maeneo ya jumuiya hiyo imetajwa ni changamoto kubwa ambayo kwa pamoja wamedhamiria kuungana kuhakikisha wanaleta amani na utulivu kwenye maeneo ambayo yameonekana kuwa na migogoro ya mara kwa mara na kushamiri kwa vikundi vya kihalifu.

“Tulihakikisha tunadhibiti vikundi vinavyotishia usalama wa wananchi wetu katika maeneo ambayo ni korofi, na hivyo kwa mara ya kwanza katika taifa letu la DRC tumefanya uchaguzi ulio huru na haki,”

Alisisitiza Rais wa jamhuri ya kidemocrasia ya congo DRC Felix Tshisekedi, ambaye amechukua mamlaka ya nchi kwa makabidhiano ya amani tangu kuasisiwa kwa taifa hilo linalotajwa kuwa na utajiri mkubwa wa madini.

VIJANA NA NAFASI KUSHIRIKI KULETA MAENDELEO

Wakati huo huo Mwenyekiti huyo aliyemaliza muda wake amezungumzia umuhimu wa nchi za jumuiya hiyo kuwashirikisha vijana katika kuleta maendeleo kwa kila nchi hasa kwa kutambua robo tatu ya wananchi wao ni vijana. Amesema hakuna sababu ya vijana kwenda nchi za Ulaya kwa ajili ya kutafuta ajira, hivyo iwekwe mikakati madhubuti ambayo itafanikisha vijana kupata nafasi ya kushiriki hatua kwa hatua kuleta maendeleo kwa nchi za jumuiya hiyo.

Related Articles

Back to top button
Close
Bongo5

FREE
VIEW