Habari

Rais Magufuli atuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha aliyekuwa RC Manyara ‘Joel Bendera’

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli ametumia salama za rambirambi kwa familia ya aliyekuwa Mkuu wa mkoa wa Manyara na Morogoro, Joel Bendera.

Soma zaidi taarifa kutoka Ikulu:

“Jioni hii nimepokea kwa mshtuko na huzuni kubwa taarifa za kifo cha Mkuu wa Mkoa Mstaafu Dkt. Joel Nkaya Bendera, natoa pole kwa familia yake na wote walioguswa na msiba huu na pia naungana nao katika kipindi hiki cha majonzi”

Hii ni sehemu ya salamu za rambirambi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli alizozitoa kufuatia kifo cha aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara Dkt. Joel Nkaya Bendera kilichotokea jioni ya leo tarehe 06 Desemba, 2017 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es Salaam alikofikishwa kwa ajili ya kupata matibabu.

Mhe. Rais Magufuli amesema Dkt. Joel Bendera atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa alioutoa kwa Taifa akiwa kiongozi katika nyadhifa mbalimbali zikiwemo Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Naibu Waziri na Mbunge na pia kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya michezo.

“Dkt. Joel Nkaya Bendera alikuwa kiongozi shupavu, mahiri na mchapakazi, alipenda kufanya kazi kwa ushirikiano na daima alitamani kupata mafanikio makubwa katika majukumu aliyokuwa nayo, hakika tutamkumbuka” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.

Pamoja na kutoa pole kwa familia ya marehemu, Mhe. Rais Magufuli amewapa pole wananchi wa Mkoa wa Manyara ambako alikuwa Mkuu wa Mkoa hadi tarehe 26 Oktoba, 2017, wananchi wa Mkoa wa Tanga ambako alikuwa Mbunge, wanachama wote wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wanamichezo wote na wote walioguswa na msiba huu na amemuombea kwa Mwenyezi Mungu aipumzishe roho yake mahali pema peponi, Amina.

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

06 Desemba, 2017

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents