Habari

Rais Magufuli kukabidhi uenyekiti wa EAC

Rais John Magufuli Jumamosi ya Mei 20, 2017 katika mkutano wa 18 wa wakuu wa Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) anatarajiwa kumkabidhi kijiti cha uwenyekiti wa jumuiya hiyo Rais wa Uganda, Yoweri Museveni baada ya Tanzania kuiongoza EAC kwa vipindi viwili mfululizo.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Balozi Augustine Mahiga katika Mkutano wa 34 wa Baraza la Mawaziri la EAC, ambapo alieleza mafanikio yaliyopatikana katika kipindi ambacho Tanzania iliiongoza jumuiya hiyo, ikiwemo kuridhia maombi ya muda mrefu ya uanachama, ya nchi ya Jamhuri ya Sudan Kusini na kuipatia uanachama kamili wa jumuiya hiyo.

“Tanzania tumemaliza muda wetu baada ya kuiongoza vipindi viwili mfululizo, Rais Magufuli Jumamosi atamkabidhi uenyekiti Rais Museveni wa Uganda,” alisema.

Kuhusu mkutano wa Baraza la Mawaziri wa EAC uliofanyika jana, alisema wajumbe wa baraza hilo watajadili ushirikiano wa masuala mbalimbali yanayohusu jumuiya hiyo, ikiwemo ushirikiano kibiashara, uwekezaji, elimu pamoja na huduma mbalimbali za kuendesha nchi wanachama hasa ujenzi wa miundombinu na uchukuzi na nishati na mengineyo kama hayo.

“Kwanza Tanzania itatoa ripoti ya ushirikiano kwa kipindi cha miaka miwili iliyoiongoza EAC ikiwemo ya ushirikiano kibiashara, kielimu na huduma za kuendesha nchi,” alisema.

Aidha alisema wajumbe hao watajadili namna ya kuondoa na au kupunguza vikwazo visivyo vya kisheria hasa vinavyokwamisha biashara ikiwemo ushuru wa forodha, vizuizi vya magari au kuzuia uzito wa magari au aina fulani za biashara, na kwamba watajadili namna ya kuanzisha soko imara la pamoja.

“Kuna vikwazo visivyo vya lazima vinavyokwamisha biashara kwa nchi wananchama, mfano Tanzania tuna vyombo viwili vinavyopima ubora wa bidhaa, TBS na TFDA ambapo wenzetu wanasema ngazi hizi mbili zinazuia biashara zao, kwa hiyo tutazungumzia suala hili. Pia tutajadili namna ya kutekeleza lengo letu la kuzuia uingizwaji wa nguo za mitumba kutoka nchi za nje ya jumuiya hii,” alisema.

Sambamba na hayo alieleza kuwa, pamoja na Rais Magufuli kukabidhi kijiti hicho kwa Museveni, Rais Mstaafu Benjamin Mkapa anatarajiwa pia katika mkutano huo kuwasilisha ripoti ya mazungumzo ya pamoja ya kuleta amani, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la wakuu wa nchi wa EAC lililotolewa mwezi Januari,2017.

Marais karibia wote watakuwepo Rais wa Kenya atakuwepo, Rais wa Uganda, Burundi, Rais Kagame atakuja, lakini Sudan wamesema wanahudhuru watatuma mwakilishi.

Na Emmy Mwaipopo

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents