Habari

Rais Magufuli kuongoza sherehe za Uhuru

Tarehe 9 Disemba Tanzania itaadhimisha miaka 55 ya Uhuru wa Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, ambapo Rais wa Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania, Dkt John Magufuli atakuwa mgeni rasmi siku hiyo.

magu-1

Ni kwa mara ya kwanza kwa Rais Magufuli kuwa mgeni rasmi katika shughuli ya maadhimisho ya sherehe za Uhuru, zinazofanyika kila mwaka wa tarehe hiyo kwa kuwa mwaka jana aliahirisha sherehe hizo na kuagiza kiasi cha fedha walichotakiwa kukitumia siku hiyo aliagiza fedha hizo zitumike kupanua Barabara ya Morocco – Mwenge jijini Dar es Salaam.

“Nchi yetu itaadhimisha sherehe za kutimiza miaka 55 ya Uhuru wa Tanzania Bara tarehe 9 Desemba, 2016. Kitaifa, maadhimisho hayo yatafanyika katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam. Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo atakuwa Dk John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” ilieleza taarifa iliyotolewa Jumatatu hii na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira, Kazi, Vijana na Watu Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama.

Kwa mujibu wa Jenista, sherehe zinazotarajiwa kufanyika siku hiyo ya kilele ya sherehe hizo ni gwaride la heshima lililoandaliwa na Vikosi vya Ulinzi na Usalama, maonesho ya Kikosi cha Makomandoo pamoja na gwaride la kimya kimya, burudani za vikundi vya ngoma za asili za mikoa ya Mbeya, Pwani, Lindi na kimoja kutoka Zanzibar.

Aidha Jenista Muhagama alisema “Kwa niaba ya serikali, natoa mwito kwa wananchi wote nchini kusherehekea siku hii kwa kuwakumbuka waasisi wetu waliotetea na kutuletea Uhuru wa nchi yetu. Niwaombe Watanzania wote katika kuadhimisha miaka 55 ya Uhuru tuunge mkono juhudi za Rais wetu Mheshimiwa Dk John Magufuli katika kuimarisha uchumi wa viwanda kwa maendeleo ya nchi yetu.”

Kauli mbiu ya kutimiza miaka 55 ya Uhuru ni “Tuunge mkono jitihada za kupinga rushwa na ufisadi na tuimarishe uchumi wa viwanda kwa maendeleo yetu.”

BY: EMMY MWAIPOPO

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents