Habari

Rais Museveni aipiga marufuku Wizara ya Utalii kuwatumia wanawake wenye maumbo makubwa kama kivutio cha utalii

Rais wa Uganda, Yoweri Museveni amesema mpango wa Wizara ya Utalii nchini humo kutaka wanawake wenye maumbo makubwa na warembo kufanya mashindano ili kuhamasisha watalii, haukubaliki na kamwe shindano hilo haliwezi kufanyika.

Rais Museveni amewaambia waandishi wa habari kuwa jambo hilo halijawahi kujadiliwa katika kikao cha baraza la mawaziri na kwamba haiingii akilini kuhamasisha watalii kwenda Uganda kwa ajili ya kuona wasichana warembo.

“Haya siyo maamuzi yaliyofanywa na baraza la mawaziri. Watu hawapaswi kuja hapa kuangalia wanawake. Sijapenda wazo hili la kuwatumia wanawake kutangaza utalii,” amesema.

Tangu kutangazwa kwa mpango huo kumekuwa na maoni mbalimbali huku baadhi ya wanawake wakiwa tayari wameanza kusambaza picha zao kwenye mitandao katika kile kinachoelezwa ‘kuwahi biashara mapema’.

Hata hivyo, mkakati huo umekuwa ukikosolewa vikali na baadhi ya makundi ya wanawake na umma kwa jumla.

Wengi wameutaja mpango huo kuwa unaodumisha hadhi ya mwanamke kama chombo cha starehe tu.

Kulingana na Waziri wa Utalii, Geofrrey Kiwanda wanawake wa jamii zote za Uganda wana maumbile ya kipekee ambayo ni nadra kuonekana sehemu zingine za dunia na ndiyo maana wanaweza kuwa kivutio kikubwa cha utalii.

Wengi wanaokosoa mpango huo wameshutumu matamshi hayo wakimtaja waziri huyo kuwa mtu aliyewavunjia heshima kwa kutaka wao kuwa kivutio cha utalii kutokana na maumbo yao.

Hata hivyo, kuna wanawake wanaodai kuwa waziri huyo hajakosea katika kujenga fikra ya kufahamisha dunia kuhusu urembo wa kiafrika ikilinganishwa na mashindano yanayowaonesha wanawake wembamba kuwa ndiyo warembo

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents