Tupo Nawe

Rais Paul Kagame arejea nchini Rwanda baada ya ziara ya siku mbili na Rais Dkt. John Pombe Magufuli iliyojikita kwenye biashara, siasa na ushirikiano

Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Mhe. Paul Kagame tarehe 07 Machi, 2019 amefanya ziara ya kikazi ya siku 2 hapa nchini ambapo amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Baada ya mazungumzo hayo Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Rais Kagame ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kufanya ziara yake ya kwanza hapa nchini tangu alipochukua kijiti cha kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo.

Kwa mujibu wa mtandao wa kijamii wa Instagram wa Ikulu, Mhe. Rais Magufuli ameeleza kuwa mazungumzo yao yamejikita katika masuala ya kiuchumi kati ya Tanzania na Rwanda pamoja na ukanda wa Jumuiya ya Afrika wenye watu zaidi ya Milioni 165, na kusisitiza umuhimu wa wana Afrika Mashariki kutilia mkazo maendeleo ya kiuchumi yenye manufaa makubwa kwa wananchi.

“Mhe. Rais Kagame nimefurahishwa sana na ujio wako, hii ni dalili nzuri ya kuendeleza na kukuza uhusiano na ushirikiano wetu, nakukaribisha tena utembelee hapa Tanzania Bara na Zanzibar pia” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Kwa upande wake Mhe. Rais Kagame amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kumkaribisha na kufanya nae mazungumzo na kwamba anatarajia mazungumzo yao kuhusu biashara, siasa na ushirikiano yatasaidia kuzijenga zaidi nchi hizo pamoja na nchi nyingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Nakushukuru kama ndugu kama rafiki, Watanzania na Wanyarwanda ni marafiki, ni ndugu, tukijijenga hapo tutaijenga Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla, kwa hiyo asante sana Mhe. Rais” amesema Mhe. Rais Kagame.

Related Articles

Back to top button
Close
Bongo5

FREE
VIEW