Michezo

Rais wa TFF atuma salamu za pongezi kwa Ngorongoro Heroes na Serengeti Boys

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania(TFF), Wallace Karia ametoa salamu za pongezi kwa timu ya Taifa ya Vijana chini ya umri wa miaka 20 (Ngorongoro Heroes) na ile ya chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) kwa kufanikiwa kufuzu katika michezo yao iliyochezwa jana huko DR Congo na Burundi.

Ngorongoro Heroes wamefanikiwa kusonga kwenye raundi ya pili na kufuzu fainali za Africa za vijana chini ya umri wa miaka 20 zitakazochezwa Niger Novemba mwaka huu baada ya kupata ushindi wa penati 5-6 dhidi ya DR Congo baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya bila kufungana kama ilivyokuwa kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa nchini Tanzania.

Wakati huo huo Serengeti Boys wenyewe wamefuzu hatua ya nusu fainali ya mashindano ya vijana ya Cecafa chini ya miaka 17 inayoendelea huko Burundi.

Rais wa TFF amesema kufanya vizuri kwa timu hizo za vijana ni faraja kubwa kwa Tanzania na inaonesha namna ambavyo TFF inaendelea kuwekeza kwenye soka la vijana.

Amesema Vijana hao wa Ngorongoro Heroes na Serengeti Boys wameonesha jitihada kubwa na wanastahili pongezi kwa jitihada hizo pamoja na jitihada za mabenchi ya ufundi ya timu hizo.

“Tumepokea matokeo ya Vijana wetu wa Ngorongoro na Serengeti Boys kwa furaha kubwa kwasababu tumekuwa tukihakikisha timu hizi zinapata maandalizi mazuri ambayo yanaonekana uwanjani kwa kupata matokeo mazuri ambayo yanailetea sifa kubwa Tanzania kwa ujumla,” amesema Karia.

Aidha Rais Karia amesema TFF itaendelea na jitihada kuzipatia maandalizi mazuri zaidi timu hizo ili ziweze kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali yanayowakabili.

Ameongeza kuwa TFF inajivunia vijana hao ambao wanaonesha mwanga mkubwa na amewaomba watu mbalimbali,Taasisi,makampuni kuunga mkono jitihada za TFF na kuiga mfano wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro waliojitokeza na kuisaidia Ngorongoro Heroes katika safari yake ya kwenda DR Congo kwenye mchezo wa marudiano.

Karia amemalizia kwa kuwashukuru wote wanaounga mkono jitihada za TFF kuendeleza mpira wa Tanzania huku akiishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais John Pombe Magufuli kwa kuunga mkono na ushirikiano wao kwa TFF.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents