Habari

Rais wa Uganda Museveni amuandikia waraka Kagame kukanusha shutuma za kulisaidi kundi linaloipinga Serikali ya Rwanda

Museveni anakanusha madai kwamba Uganda inalisaidia kundi la upinzani la wanasiasa wanaoishi uhamishoni la Rwanda National Congress wanaoipinga serikali ya Kagame.

Kwa mujibu wa DW. Katika waraka uliochapishwa katika gazeti linalothibitiwa na serikali ya Uganda la The New Vision, Rais Museveni alisema serikali haijahusika kabisa katika kulisaidia kundi hilo la upinzani.

Rais Museveni, aliandika katika barua hiyo kwamba alikutana na mwanachama wa kundi hilo aliyezungumza mambo mabaya yanayoendelea Rwanda na aliomba serikali yake imsadie.

Vile vile Museveni alieleza katika siku tofauti aliwahi kukutana na mfanyabiashara tajiri wa Kirwanda anayeishi uhamishoni nchini Uganda Tribert Rujugiro ambaye serikali ya Rwanda inamshutumu kwa kuwafadhili waasi wanaoipinga serikali ya Kagame, kwa mujibu wa barua hiyo ya Museveni aliyomuandikia rais Kagame.  

Kimsingi Rujugiro anakanusha kuunga mkono makundi yanayompinga Kagame ambapo ameliambia gazeti la New Vison siku ya Jumapili kwamba hata rais Kagame binafsi anajua kwamba ikiwa ataamua kuwasaidia waasi wapambane dhidi yake basi itachukua chini ya kipindi cha miezi sita kumuangusha.

Katika barua ya Museveni rais huyo wa Uganda alilikataa ombi la Rwanda linalomtaka kumfurusha na kufunga biashara za Mfanyabiashara huyo tajiri, Rujugiro anayemiliki kiwanda cha Tumbaku nchini Uganda na badala yake kuitaka Rwanda kumfungulia mashtaka ya ugaidi  na  iwapo mahakama itathibitisha tuhuma zinazomkabili mfanyabiashara huyo basi Uganda itazuilia mali zake.

Mvutano baina ya Rwanda na Uganda hauonekani kumalizika.

Barua hiyo inajiri wakati hofu na mvutano unaendelea kuchacha baina ya mataifa haya mawili jirani katika Afrika ya Mashariki.

Duru za kuaminika zimethibitisha  kwamba ni kweli barua hiyo iliandikwa na rais Museveni kwa lengo la kumsafia nia rais wa Rwanda Kagame anayeamini  serikali ya Uganda inalisaidia kundi hilo la wapinzani wa Kagame linaloongozwa na aliyekuwa wakati mmoja mkuu wa jeshi la Rwanda Kayumba Nyamwasa.

Ruandischer Dissident Faustin Kayumba Nyamwasa (STEPHANE DE SAKUTIN/AFP/GettyImages)

Aliyekuwa mkuu wa jeshi Rwanda Kayumba Nyamwasa

Nyamwasa anayeishi mafichoni nchini Afrika Kusini alinusurika majaribio mawili ya kuuliwa anayoamini yalipangwa na viongozi wakuu nchini Rwanda, serikali ya Rwanda ilikanusha madai hayo.

Mvutano baina ya Rwanda na Uganda umeendelea kukua sambamba na mvutano uliopo kati ya Rwanda na Burundi na kulingana na  wachambuzi hali hii inaweza kusababisha kuzuka kwa mgogoro mwingine wa mapambano Mashariki mwa Kongo.

Rais Museveni na Kagame hivi karibuni wamekuwa wakitoa kauli za kutishiana, Uganda ikisema wanaojaribu kuisambaratisha hawajui uwezo walio nao nayo Rwanda ikijibu kwamba hakuna mtu anayeweza kuiporomosha.

Serikali ya Rwanda ilifunga mpaka wake na Uganda na pia kuwaamrisha raia wake wasisafiri kwenda Uganda.

Tofauti za mataifa hayo ni tangu mwaka 1990 ambapo majeshi yao yaliingia katika vita Mashariki mwa Kongo na kila moja kusaidia kundi pinzani la waasi.

By Ally Juma.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents