Habari

Rais wazamani Misri, Mohammed Morsi aaga dunia ghafla mahakamani 

Aliyekuwa rais wa Misri, Mohammed Morsi, aliyeng’olewa madarakani na jeshi mnamo 2013 ameaga dunia ghafla akiwa mahakamani, televisheni ya taifa hilo imetangaza.

Mahakama nchini Misri ilibatilisha hukumu ya kifo mnamo 2016 dhidi ya rais huyo aliyepinduliwa.

Kwa mujibu wa shirika la habari la BBC, Morsi alikumiwa kifo baada ya kulaumiwa kuhusika na kutoroka kwa wafungwa wengi wakati wa mapinduzi ya mwaka 2011 nchini humo.

Alichaguliwa kuwa rais mwaka 2012 lakini akaondolewa katika mapinduzi ya jeshi mwaka mmoja baadaye, kufuatia maandamano makubwa ya kupinga utawala wake.

Morsi alishahukumiwa kifungo cha maisha jela kwa mashtaka yanayohusu ugaidi.

Umauti umemkuta alipokuwa mahakamani akisikiliza mashtaka dhidi yake ya kujihusisha kijasusi na kundi la kiislamu la Hamas la nchini Palestina.

Kwa muda wote, Morsi na wafuasi wake wamekuwa wakishikilia msimamo kuwa mashtaka dhidi yake yamechochewa na uhasama wa kisiasa baina yake na uongozi uliopo kwa sasa.

Mtoto wa kiume wa Morsi, Abdullah hivi karibuni alilamikia juu ya baba yake kunyimwa huduma muhimu za kiafya akiwa gerezani.

Aliliambia shirika la kimataifa la habari la AP mwezi Oktoba mwaka jana kuwa baba yake amekuwa akifungiwa muda mwingi kwenye seli ya peke yake na kunyimwa matibabu ya magonjwa yanayomsumbua shinikizo la damu na kisukari.

Miezi mitano nyuma, Abdullah alichapisha maoni yake katika gazeti mashuhuri nchini Marekani na kudai kuwa mamlaka zilikuwa “zikifanya hivyo kwa makusudi, sababu walitaka ‘afe kwa sababu za kawaida’ haraka iwezekanavyo.”Mohammed Morsi

Morsi ni nani?

Mohammed Morsi alizaliwa katika kijiji cha El-Awwadh katika jimbo lililopo kwenye delta za mto Nile la Sharqiya mwaka 1951.

Alisomea Uhandisi katika chuo Kikuu cha Cairo katika miaka ya 70 kabla ya kuhamia nchini Marekani ambapo alitunukiwa Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Uhandisi.

Morsi aliweka rekodi ya kuwa kiongozi wa kwanza kuchaguliwa katika uchaguzi wa haki na huru mwaka 2012, akiwa kiongozi mwandamizi wa kundi la kiislamu la Muslim Brotherhood ambalo limepigwa marufuku kwa sasa nchini humo.

Hata hivyo utawala wake ulikumbwa na wimbi la maandamano ya wanaharakati ambao walimshutumu yeye na kundi la Muslim Brotherhood kujilimbikizia madaraka.

Baada ya maandamano kuwa makubwa, na wafuasi wa Morsi kushambulia wapinzani wake, jeshi likiwa chini ya rais wa sasa Abdel Fattah el-Sisi liliendesha mapinduzi na kumng’oa Morsi madarakani, Juni 2013.

Jeshi liliendelea kupambana na wafuasi wa Morsi baada ya mapinduzi, na zaidi ya wafuasi wake 1,000 waliuawa Agosti 2013.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents