Uncategorized

Rais Yoweri Museveni kugombea urais kwa mara ya sita, chama chake chamteua kuwania tena mwaka 2021

Chama tawala nchini Uganda kimemteua Rais Yoweri Kaguta Museveni kuwa mgombea wake wa urais katika uchaguzi wa mwaka 2021.

Hii inamaana ya kuwa, kiongozi huyo mwenye miaka 74, na aliyeingia madarakani kwa mtutu wa bunduki mwaka 1986, atagombea urais kwa muhula wa sita.

Kwa mujibu wa shirika la habari la BBC, Chama cha National Resistance Movement (NRM) kimekubali, katika kikao kilichoongozwa na Museveni jana Jumatano kuwa ” (Museveni) aendelee kuongoza harakati na taifa mwaka 2021 na kuendelea ili kuondosha vikwazo vya mabadiliko na maendeleo.”

Miaka ya nyuma, Museveni aliwahi kusema kuwa, viongozi “wanaodumu” madarakani ndio chanzo cha matatizo barani Afrika.

Hata hivyo, wakati akigombea muhula wa tano wa madaraka mwaka 2016, alisema kuwa huo haukuwa muda muafaka kwake kuondoka madarakani kwani bado alikuwa na kazi ya kufanya.

Ugombea wake katika uchaguzi ujao unakuja baada ya kusaini kuwa sheria mswada ambao uliondoa ukomo wa urais wa miaka 75.

Hata hivyo, kupitishwa kwa muswada huo bungeni kuligubikwa na vurumai kubwa kutokana na kupingwa na wabunge wa upizani.

Mahakama ya Upeo ya Uganda mwezi wa Januari imeanza kusikiliza shauri la kupinga mabadiliko hayo ya sheria.

Ilifikia mahala makonde yalirushwa ndani ya bunge baina ya wabunge wa upinzani na maafisaa usalama ambao wanaaminika ni kutoka kikosi cha ulinzi wa rais.

Upinzani dhidi ya mabadiliko hayo ya sheria yamemuibua msanii Bobi Wine kama kinara wa upinzani na mwiba mkali dhidi ya serikali ya Museveni ndani na nje ya bunge la Uganda.

Tangazo la Museveni kugombea tena lilitarajiwa kutkana na mabadiliko ya sheria lakini wachambuzi wameshangaa kutolewa miaka miwili kabla ya uchaguzi wenyewe.

Kainerugaba Muhoozi

Luteni Jenerali Kainerugaba Muhoozi anadaiwa kupikwa ili amrithi baba yake Yoweri Museveni uraisi wa Uganda

Wiki hii pia rais Museveni amempandisha cheo mwanawe wa kiume na kufikia cheo cha pili kwa ukubwa zaidi jeshini.

Kainerugaba Muhoozi sasa amepanda kutoka kuwa Meja Jenerali na kufikia Luteni Jenerali katika jeshi la Uganda. Ndani ya miaka sita iliyopita, Jenerali Muhoozi amepanda vyeo mara tatu.

Japo amekuwa mkuu wa vikosi maalumu vya jeshi la Uganda na sasa anahudumu kama mshauri wa rais wa operesheni maalumu, upandaji wake wa vyeo unaonekana ni wa kasi kubwa.

Kasi hiyo ndiyo ambayo wakosoaji wa rais Museveni na wanaharakati wanadai ni kielelezo kuwa kuna mipango unaosukwa wa mtoto huyo wa rais kumrithi baba yake.

Hata hivyo, Jenerali Muhoozi amekuwa akikanusha kuwa ana mipango ya kujiingiza kwenye masuala ya siasa.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents