Tupo Nawe

RC Makonda atoa zawadi kwa askari waliohatarisha uhai wao kwa maslahi ya Taifa (Video)

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda leo amewatunuku vyeti na zawadi za Pikipiki,Saruji, Mabati,fedha na vifaa vya ndani kwa Askari polisi wazalendo waliofanya vizuri katika kazi yao na kuwataka Askari wengine kujituma kwa moyo mmoja kulinda usalama wa raia na Mali zao.

Mgawanyo wa Zawadi alizokabidhi RC Makonda umehusisha makundi mbalimbali ikiwemo Askari waliojeruhiwa wakipambania uhai wa watu, Wajane ambao waume zao walifariki wakitekeleza majukumu ya kazi, Askari waliohatarisha maisha yao kwa maslahi ya taifa pamoja na raia wanaofanya kazi nzuri na Jeshi la Polisi ambapo amewapongeza askari kwa kazi nzuri wanayofanya.

Aidha RC Makonda amesema anajivunia kuona matukio ya uhalifu yamemalizika katika Mkoa wa Dar es salaam tofauti na siku za nyuma ambapo yalishuhudiwa matukio ya kusikika milio ya bunduki, uvamizi wa bank, uvamizi wa vituo vya polisi, uporaji na panya road waliokuwa wakitishia usalama.

RC Makonda amesema ataendelea kuliongezea nguvu jeshi hilo kwa kuhakikisha anapambana kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili ili kuhakikisha Jiji la Dar es salaam linaendelea kuwa salama wakati wote.

Pamoja na hayo RC Makonda amemtaka kamanda wa polisi kanda maalumu Lazaro Mambosasa kuangalia kama sheria inaruhusu jeshi la polisi kuanza kuyatumia magari yaliyotelekezwa na wahalifu mbalimbali ili magari hayo yatumike kufanya kazi za jeshi hilo kwa manufaa ya wananchi badala ya kuyaacha yazidi kuharibika na kuoza.

Baada ya hafla ya mchana kumalizika RC Makonda atakutana tena na askari polisi katika hafla ya chakula cha jioni na burudani mbalimbali ambapo pia atawakabidhi Zawadi ya magari mawili askari wa kiume na wa kike waliofanya kazi nzuri.

Related Articles

Back to top button
Close
Bongo5

FREE
VIEW