Habari

RC Mnyeti atoa agizo kukamatwa kwa mbunge huyu

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti amemuagiza mkuu wa wilaya ya Kiteto, Mhandisi Tumaini Magessa kumkamata mbunge wa Kiteto (CCM), Emmanuel Papian endapo atabainika kuwa anachochea migogoro ya ardhi.

Mnyeti amesema hayo Ijumaa Januari 19, 2018 wakati akihitimisha ziara yake ya siku saba alipotembelea wilaya ya Kiteto.

Amesema endapo Papian anasababisha migogoro ya ardhi kwa kuchochea wananchi walime kwenye hifadhi, anapaswa kuchukuliwa hatua.

“Mkuu wa wilaya wewe ndiye mteule wa Rais kwenye eneo hili la Kiteto. Endapo mtu mwingine hata kama ni mbunge wa jimbo akiwa anachochea migogoro ya ardhi, uwe unawakamata na kuwaweka ndani,” amesema Mnyeti.

Amesema migogoro ya ardhi kwenye wilaya ya Kiteto haitaweza kumalizika endapo wanasiasa wataendelea kuwachonganisha wakulima na wafugaji.

“Mbunge asiote mapembe na kupanda kichwani kwako, wewe ndiye mtawala wa hapa. Nataka siku nyingine unipigie simu kuwa umemkamata na kumweka ndani mbunge ili asirudie hilo,” amesema Mnyeti na kuongeza,

“Mkuu wa wilaya unapozungumzia mgogoro wa kijiji zungumza sehemu husika na kama mbunge akiendelea kuchochea umkamate,” amesema Mnyeti.

Akizungumza kwa njia ya simu na Mwananchi, Papian hakukubali wala kukataa juu ya yeye kuchochea na kusababisha migogoro ya ardhi, ila amesema muda utaongea.

“Hapa tunavyozungumza nipo kwenye gari, ila suala hilo uliloniuliza litajulikana huko mbeleni tunakokwenda hivyo tujipe muda tuu itabainika,” amesema Papian.

Chanzo; Mwananchi

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents