Michezo

Rekodi za Messi zinatisha, rasmi afikisha magoli 700 miguu bado inahamu ya kucheka na nyavu

Rekodi za Messi zinatisha, rasmi afikisha magoli 700 miguu bado inahamu ya kucheka na nyavu

Lionel Messi amefikisha jumla ya magoli 700 hapo jana baada ya kufunga bao moja katika mchezo uliyomalizika kwa sare ya 2 – 2 dhidiya Atletico de Madrid.

Kabla ya mchezo huo, Messi alikuwa na jumla ya magoli 699 ambayo amefunga kwenye michezo yake yote tangu kuanza kwake soka ikiwemo yale ya timu ya Taifa ya Argentina.

Ndani ya Barcelona, Messi amefunga magoli 630 kwenye mechi 724 alizoitumikia klabu hiyo, mabao 70 kwenye timu yake ya Taifa ya Argentina.

Goli lake la kwanza akiwa ndani ya Barça amefanikiwa Mei 1, 2015 kwenye mchezo dhidi ya Albacete.

Kunako Ligi kuu ya Hispania, Messi amefunga jumla ya magoli 441 katika mechi 480 alizocheza ndani ya LaLiga. Mabao 114 kwenye mechi 141 alizocheza Champions League.  Magoli 53 katika michezo 75 ya Copa del Rey. Mabao 3 katika mechi 4 za fainali ya European Super Cup. Mabao 5 kwenye michezo 5 aliyocheza Club WorldCup na magoli 14 kwenye mechi 19 ambazo amecheza katika michuano ya Spanish Super Cup.

Messi alifanikiwa kufunga goli lake la kwanza akiwa katika timu ya Taifa ya Argentina mwezi Machi mwaka 2006 dhidi ya Croatia ikiwa ni mchezo wa kirafiki na mchezo wa mashindano alitupia bao lake la mwisho akiwa analitumikia taifa lake ilikuwa Novemba 2019 mchezo dhidi ya Uruguay.

Messi ameshinda mataji 10 ya LaLiga, mataji manne (4) ya Champions Leagues na Ballon d’Ors sita (6).  Lionel Messi amefunga ‘hat-trick’ ama zaidi ya magoli manne kwenye michezo zaidi ya 54 ikiwa ni ndani ya klabu na Argentina.

Amewahi kufunga magoli matano (5) ndani ya mchezo mmoja tu, ulikuwa wa Champions Leaguega msimu wa mwaka 2011-1 dhidi ya Bayer Leverkusen wakati mwaka 2012 akiandika rekodi ya kufunga magoli 91.

Kunako mwezi Oktoba 2014, Messi alitangazwa kuwa mfungaji wa muda wote wa LaLiga akivunja rekodi iliyoachwa na Telmo Zarra alipokua akiichezea Athletic Club kati ya mwaka 1940 hadi 1955 alipofunga magoli 251.

Kwa sasa Zarra anashikilia nafasi ya tatu, namba mbili ikishikiliwa na Cristiano Ronaldo ambaye kunako LaLiga amefanikiwa kufunga jumla ya magoli 311 katika mechi 292 alizocheza kwenye ligi hiyo akiwa Real Madrid kuanzia mwaka 2009 hadi 2018.

Kwa sasa akiwa Juventus nchini Italia, Ronaldo amefikisha jumla ya magoli 728 (kwenye michezo yake 1005, yakiwemo mabao 99 kwenye mechi alizocheza akiitumikia timu yake ya taifa ya Ureno).

Hivyo basi kutokana na kulinganisha idadi ya magoli, na rekodi za zama mbalimbali kwenye mchezo wa soka ni Wachezaji saba (7) pekee waliofanikiwa kufikisha idadi hiyo ya magoli 700.

Aliyekuwa mshambuliaji wa Austalia, Josef Bican alifunga jumla ya magoli 805 kati ya mwaka 1930 hadi 1950s.

Mchezaji wa zamani wa Barcelona, Romario alifunga magoli 772 ingawaje wapo watu wanaodai kuwa takwimu hizo zina kasoro huku Mbrazil mwenzake Pele akifunga mabao  767.

Aliyekuwa mshambuliaji wa Real Madrid, Ferenc Puskas ambaye alitangaza kustaafu mwaka 1966 kwa upande wake alifunga jumla ya magoli 746g, wakati Mjerumani Gerd ‘Der Bomber’ Muller akifunga mabao 735 na kuatangaza kustaafu mwaka 1981.

Messi na Ronaldo bado wanaendelea kusakata kabumbu tena kwenye levo za juu kabisa hivyo tunategemea huwenda wanaweza kuvunja rekodi za zama hizo na kuandika mafanikio makubwa zaidi.

Wakati ndiyo kwanza Messi amefikisha miaka 33 mwezi huu uliyopita Juni 24 amefanikiwa kuandika rekodi nyingi ikiwa pamoja na kufikisha idadi hiyo ya magoli 700, Wapenzi wa soka tunatarajia mengi kuyaona na kuyashuhudia kutoka kwa Muargentina huyo.

Imeandikwa na Hamza Fumo

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents