Richmond yafanya utapeli mwingine

KAMPUNI ya Richmond Development Company LLC imezidi kuonesha taswira yake ya kisanii baada ya uchunguzi wa gazeti hili kubaini kuwa hivi sasa imeanza kufanya utapeli mwingine

Na Mwandishi Wa Majira




KAMPUNI ya Richmond Development Company LLC ambayo ilishindwa kukamilisha mradi wa megawati 100 wa umeme wa dharura nchini imezidi kuonesha taswira yake ya kisanii baada ya uchunguzi wa gazeti hili kubaini kuwa hivi sasa imeanza kufanya utapeli mwingine kwa kutumia jina la Tanzania.

Kwa mujibu wa habari ambazo Majira Jumapili imezipata, viongozi wa Richmond hasa walioko Marekani, Bw. Mohammed Gire na Dkt. Mohammed Huque, wamekuwa wakiutumia mradi wa umeme wa dharura uliowashinda wa Ubungo hapa nchini ili kupata mikataba mingine minono duniani.

Gazeti hili lilithibitisha taarifa hizo kupitia tovuti ya kampuni hiyo yenye anuani ya www.rdevco.com, ambapo ukifungua kiunganishi cha ‘recent projects’ (miradi ya hivi karibuni) bila aibu Richmond inajinasibu duniani kuwa mwaka 2006 walikamilisha mradi huo kwa ufanisi katika zile megawati 25 za kwanza.

“Mwaka 2006, tulikamilisha mradi wa umeme wa dharura wa Ubungo, Dar es Salaam, Tanzania. Tuliukamilisha mradi huo kihandisi, kimanunuzi na kiuendeshaji kwa zile megawati 25 za kwanza,” inasema taarifa ya tovuti hiyo.

Lakini taarifa za hakika zilizokusanywa na Kamati Teule ya Bunge iliyoongozwa na Mbunge wa Kyela (CCM), Dkt. Harrison Mwakyembe, zinaonesha kuwa ni Dowans ndio waliofunga na kuwasha megawati 25 za kwanza, huku Richmond wakiwa ndio waliouleta mtambo huo lakini ukawashinda kuufunga.

Oktoba 30, 2006 Richmond baada ya mvutano wa muda mrefu na TANESCO, taarifa za Kamati ya Bunge zinaonesha, ndipo walipoleta nchini mtambo wa megawati 22 tu ambao hata hivyo ulikaa bila kufungwa kwa muda mrefu hadi Novemba 14 vilipowasili viunganishi vyake.

Ripoti ya Kamati ya Bunge pia ikimkariri Mhandisi Boniface Njombe, ambaye alikuwa Meneja wa Mradi huo kwa upande wa TANESCO akikiri kuwa Richmond walionekana hawana hata utaalamu wa kufunga mashine na mara kadhaa walikosea kiasi cha kusababisha mlipuko.

Tofauti na Richmond wanavyojinadi kwenye tovuti hiyo, uchunguzi wa gazeti hili umezidi kuonesha kuwa baadaye Dowans, ambao walichukua rasmi kazi za Richmond kuanzia Desemba 23, ndio waliosimamia hadi mtambo huo ukatengemaa na kuanza rasmi kuzalisha umeme mwanzoni mwa 2007, tofauti na tovuti hiyo inavyosema ulikamilika 2006.

Katika tovuti hiyo Richmond pia inajitangaza kuwa ndiyo iliyoandaa taratibu zote kwa ajili ufungaji wa mtambo uliokamilisha uzalishaji wa megawati 100 za umeme jambo ambalo kwa mujibu wa ripoti rasmi za Bunge si la kweli pia kwani tangu Desemba 2006 Dowans ndio walioshika kazi zote za kihandisi na kimanunuzi na ndio wanaolipwa hadi sasa.

Katika hatua nyingine, imebainika kuwa tofauti na awali ilipokuwa ikitangaza kwenye tovuti hiyo kuwa ina mradi wa ujenzi wa uwanja wa mpira wenye uwezo wa kuchukua watu 65,000 katika eneo la Afrika Mashariki, ukarabati wa viwanja vya ndege na ujenzi wa bomba la mafuta, hivi sasa matangazo hayo yameondolewa kwenye tovuti hiyo bila maelezo yoyote.

Kuwepo kwa matangazo hayo yaliyokuwa yakitaja miradi ya uongo au ambayo kampuni hiyo iliishindwa ni moja ya mambo yaliyowapa watanzania wengi shaka kiasi cha kushinikiza kampuni hiyo ichunguzwe kuona iwapo ilikuwa na sifa ilizokuwa ikijigamba nazo.

Juhudi za gazeti hili kuwasiliana na viongozi wa Richmond walioko nchini Marekani hazikuzaa matunda.

Awali gazeti hili lilijaribu kupiga simu ya kampuni hiyo lakini mara zote simu hiyo ilikuwa ikielezwa kuwa haipo au imeshindwa kuunganishwa.

Lakini hadi jana ikiwa ni wiki mbili tangu gazeti hili lilipomtumia maswali kupitia anuani ya baruapepe ya kampuni yake kuomba ufafanuzi juu ya masuala hayo, Bw. Gire hakujibu chochote.

Hivi sasa Serikali iko katika mchakato wa kuwachukulia hatua za kinidhamu watumishi wote wa umma waliohusika katika kuipa zabuni kampuni hiyo.

Sakata hilo pia lilisababisha aliyekuwa Waziri Mkuu, Bw. Edward Lowassa pamoja na waliokuwa mawaziri waandamizi, Dkt. Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi kujiuzulu kutokana na kuhusishwa na kashfa hiyo.

Kuendelea kwa Richmond kung’ang’ania mradi wa Ubungo wa kufua umeme wa dharura, kunaweza kufasiriwa kuwa ni kuzidi kuiumbua kampuni hiyo lakini pia wachunguzi wengine wa mambo, wanapata shaka kuwa huenda madai kuwa kampuni hiyo bado inanufaika au inajihusisha na mradi huo kupitia kampuni ya Dowans yakapata nguvu.

Dowans ambayo ililetwa na Richmond ikiwa haifahamiki hapa nchini wala miongoni mwa makampuni makubwa ya nishati, imekuwa ikilipwa mamilioni na Serikali kupitia TANESCO kwa mkataba huo iliourithi.


 


Source: Majira

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents