Habari

Risasi bar, ni Dar jana usiku

Bar moja Jijini Dar es Salaam imegeuzwa uwanja wa mapambano baada ya majambazi yenye silaha kuibuka ghafla na kuanza kumwaga risasi mtindo mmoja.

Na Mwandishi Wa Alasiri, Jijini



Bar moja Jijini Dar es Salaam imegeuzwa uwanja wa mapambano baada ya majambazi yenye silaha kuibuka ghafla na kuanza kumwaga risasi mtindo mmoja.


Katika tukio hilo, wateja waliokuwa wakijinafasi kwa raha zao waliwekwa chini ya ulinzi na kuporwa pesa, simu na dhahabu. Pia fedha za mauzo zimeporwa na majambazi hayo ambayo pia yalijeruhi mtu mmoja kwa risasi.


Taarifa za kipolisi zilizopatikana leo asubuhi zinasema tukio hilo limejiri mishale ya saa moja na saa mbili usiku jana, pale kwenye bar maarufu ya Flamingo iliyopo Boko, nje kidogo ya Manispaa ya Kinondoni.


Kwa mujibu wa taarifa hizo toka polisi, majambazi hayo yalitua kwenye bar hiyo yakiwa na gari dogo aina ya Toyota `Baloon`, ambalo hata hivyo, namba zake hazikuweza kupatikana mara moja.


Zikasema taarifa hizo kuwa majambazi hayo yalisimamisha gari yao karibu na mlinzi wa bar hiyo aitwaye Seif Kipara, ambaye muda huo alikuwa amekamata bunduki aina ya Mark III iliyokuwa na risasi nne.


Ikaelezwa zaidi kuwa baada ya kusimamisha gari, majambazi hayo yakamvamia ghafla mlinzi huyo wa Kampuni ya Regimental, kumteka nyara kabla ya kumpiga risasi moja tumboni kwa kutumia bastola yao. Baadaye inasemekana yalimpora silaha yake na kisha kujitoma ndani ya bar hiyo.


Kikasema chanzo chetu kuwa majambazi hayo yaliwaweka wateja wote chini ya ulinzi na kuelekea kaunta ya baa hiyo ambako yalimshambulia mhudumu wa Bi. Mwajab Abdallah na kupora shilingi 450,000 za mauzo ya siku hiyo.


Wakati huohuo, mwanamke mmoja mkazi wa Yombo Makangarawe, Scolastika Richard anadaiwa kutoroka na Shilingi 3,610,000 mali ya mumewe.


Kaimu Kamanda wa mkoa wa kipolisi wa Temeke, Leornad Muyi amesema mtoa taarifa aliripoti kutoweka kwa fedha hizo jana saa 6.30 mchana.


Akasema mbali ya kuondoka na fedha hizo, mwanamke huyo alitoweka na watoto wawili pamoja na mfanyakazi wa ndani.


Hata hivyo, kamanda huyo hakutoa ufafanuzi zaidi kuhusiana na tatizo hilo.


Source: Alasiri

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents