Habari

Rufaa ya Nyari kuanza kusikilizwa Agosti 20

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, imepanga kusikiliza rufaa ya kupinga kifungo cha miaka 30 jela dhidi ya mfanyabiashara mashuhuri wa mjini hapa, Justine Nyari iliyotolewa mwaka 2005.

Na Mwandishi Wa Mwananchi, Arusha


MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, imepanga kusikiliza rufaa ya kupinga kifungo cha miaka 30 jela dhidi ya mfanyabiashara mashuhuri wa mjini hapa, Justine Nyari iliyotolewa mwaka 2005.


Rufaa hiyo iliyowasilishwa mwaka huo huo na mawakili wake, Loom Ojare na Midan Mwale, imepangwa kusikilizwa na Jaji Othman Chande wa Mahakama Kuu kuanzia Agosti 20.


Nyari ni mfanyabiashara mashuhuri anayemiliki vitega uchumi kadhaa ikiwamo Kampuni ya ununuzi wa madini ya Tanzanite ya J.N Mining ambayo ni moja kati ya kampuni zilizokuwa zikifanya vizuri katika biashara hiyo.


Kadri siku zinavyokaribia usikilizwaji wa rufaa hiyo, kumekuwepo na hisia na minong’ono mjini hapa ambayo iliongezewa nguvu na taarifa ya gazeti moja iliyokuwa na kichwa cha habari cha ‘Nyari Huru’


Gazeti hilo linalochapwa jijini Arusha liliandika kwa kirefu rufaa hiyo na kudai kuwa baadhi ya marafiki na wafuasi wake wanasubiri kwa hamu kumuona akirejea mitaani.


Hata hivyo taarifa za gazeti hilo zimezua hisia tofauti miongoni mwa wafanyabiashara hasa wenye asili ya kiasia waliokuwa wakijishughulisha na biashara ya Tanzanite ambao wameonekana wakiwa katika makundi kutafakari.


Haijaelezwa hasa nini sababu zinazowafanya wafanyabiashara hao wakae katika makundi, lakini wakili mmoja alisema mahakama haiendeshwi kwa taarifa za magazeti bali mwenendo mzima wa shauri.


Akitoa hukumu dhidi ya Nyari na Banjoo, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa Arusha, Irvin Mgeta, aliamuru pia kutaifishwa mara moja kwa gari aina ya Corolla lenye namba za usajili TZL 9500 lililotumika katika uporaji huo.


Hata hivyo mahakama ilimuachia huru mshtakiwa wa pili ambaye ni Afisa Madini Kanda ya Kaskazini,Teddy Goliama, aliyekuwa akitetewa na wakili Alute Mughway baada ya kukosekana ushahidi.


Hakimu alifafanua kuwa ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka uliotolewa mahakamani hapo umeweza kuithibitishia mahakama bila shaka yoyote kuwa Nyari na Banjoo walipanga na kushiriki katika uporaji huo.


Washtakiwa walitiwa hatiani kwa kupora fedha taslimu Sh10 milioni na madini yenye thamani ya Sh30 milioni mali ya Kampuni ya River Gems (T) Ltd iliyopo mtaa wa Goliondoi Desemba 6, 2002


Alisema mahakama imeridhika juu ya tukio hilo lililotokea saa 12.30 asubuhi, Nyari akiwa na shahidi wa tano wa upande wa mashtaka, James Njoroge, walimkabidhi mshtakiwa wa tatu begi lililokuwa na bastola zilizotumika katika tukio hilo.


Alifafanua kuwa ushahidi huo unaunganika na wa Chales Mushi, aliyeiambia mahakama kuwa siku hiyo alipewa simu na John Mhala ili afuatilie kwa karibu saa za kufunguliwa kwa ofisi za River Gems ili naye amtaarifu Nyari.


Ushahidi huo unaonyesha kuwa mara tu baada ya kufunguliwa kwa ofisi hizo, Mushi alimtaarifu Nyari ambaye alimuuliza kama mshtakiwa wa tatu (Banjoo) alikuwa ameshafika eneo hilo naye akamjibu kuwa alikuwa hajafika.


Alisema ushahidi wa Edgar Minja na Simon Minja waliokuwa wafanyakazi wa kampuni hiyo, unaonyesha kuwa waliweza kumtambua mshtakiwa wa tatu wakati akiegesha gari aina ya Corrola iliyotumika katika uporaji huo.


Source: Mwananchi

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents