Habari

Rwanda yawazika wahanga 85,000 wa mauaji ya kimbari

Mabaki ya karibu watu 85,000 waliouawa katika mauaji ya kimbari nchini Rwanda yamezikwa Jumamosi mjini Kigali, robo karne baada ya mauaji hayo. Waombolezaji walimamia wakati majeneza 81 yakizikwa mjini Kigali.

Ruanda Beisetzung Opfer Völkermord von 1994 (Getty Images/AFP/Y. Chiba)
Wamaume wakibeba majeneza 81 ya mabaki yaliogunduliwa ya wahanga 84,437 wa mauaji ya kimbari ya 1994, tayari kwa ajili ya kuzikwa mjini Kigali, Mei 4, 2019.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Deutsche Well, na The East African Waombolezaji walisimama wakati majeneza 81 yenye mabaki ya waathirika 84,437 wa mauaji ya halaiki ya mwaka 1994 wakizikwa kwenye kituo cha kumbukumbu ya mauaji ya kimbari cha Nyanza mjini Kigali.

Walikuwa miongoni mwa watu zaidi ya 800,000, wengi wao Watutsi, waliouliwa kwa muda wa zaidi ya siku 100 na Wahutu wenye msimamo mkali pamoja na vikosi vya wanamgambo vilivyodhamiria kuisafisha jamii ya wachache wa kabila la Watutsi nchini Rwanda.

Rwanda huanza kumbukumbu za mauaji ya kimbari kila Aprili 7 – siku ambayo mauaji hayo yalianza. Lakini mwaka huu imeshuhudia kumbukumbu makhsusi kuadhimisha miaka 25.

“Kumbukumbu ya mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi ni wajibu wa kila Mnyarwanda — na hivyo ndivyo ilivyo katika kuwapa maziko ya heshima,” alisema waziri wa sheria Johston Busingye wakati wa maziko ya siku ya Jumamosi.

Ruanda Beisetzung Opfer Völkermord von 1994 (Getty Images/AFP/Y. Chiba)

Watu wakiandaa majeneza yalio na mabaki ya wahanga 84,437 wa mauaji ya kimbari yaliogunduliwa hivi karibuni, kabla ya maziko yaliofanyika Mei 4 mjini Kigali.

“Angalau najua pa kuweka shada la maua”

Baadhi ya waombolezaji waliangua vilio wakati manusura wakizungumzia maumivu ya kuwapoteza wapendwa wao kwa njia ya kikatili. Idadi kadhaa walisindikizwa na waongozaji.

Emmanuel Nduwayezu alisema ugunduzi huo unamaanisha hatimaye alipata mahala pa kuja kila Aprili 7, na kuweka shada la maua katika kumbukumbu ya familia yake iliyouawa.

“Hivi sasa nina furaha kwa sababu nimemzika baba yangu, dada yangu na watoto wake, na shemeji yangu. Miaka 25 imepita na sikuwa najuwa wapi walipo,” aliliambia shirika la habari la AFP.

“Kila siku nilikuwa nawafikiria na kuchanganyikiwa (kuhusu) wapi alipo baba yangu lakini sasa nimempata na nimemzika.”

Mabaki ya watu waliozikwa Jumamosi yalipatikana mwaka uliopita, wakati ambapo mashimo 143 yaliokuwa na maelfu ya mifupa na vipande vya nguo yalipogunduliwa chini ya makaazi kwenye kingo za mji wa Kigali.

Wale waliofukuliwa kwa ajili ya maziko Jumamosi walitoka kwenye mashimo 43 kama hayo – kukiwa bado na mengine zaidi 100. Juhudi zilifanyika ili wanafamilia waweze kuwatambua wapendwa wao kupitia meno yao, mavazi na ishara nyingine. Wameungana na waathirika wengine 11,000 waliozikwa tayari kwenye kituo cha kumbukumbu cha Nyanza.

Jean-Pierre Dusingizemungu, kiongozi wa Ibuka, ambalo ni Shirika la Manusura wa mauaji ya kimbari, alisema mmiliki wa nyumba katika eneo hilo alifichua eneo la makaburi hayo pale tu alipotishiwa kukamatwa.

Ruanda Beisetzung Opfer Völkermord von 1994 (Getty Images/AFP/Y. Chiba)

Wanaume wakibeba majeneza yenye mabaki ya wahanga wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 tayari kwa maziko kwenye kituo cha kumbukumbuku cha Nyanza mjini Kigali, Rwanda, Mei 4.

Mashimo zaidi yaligunduliwa baadae wakati mwanaume, aliyepewa jukumu mwaka 1994, la kutupa miili, alipojitokeza na taarifa mpya. Dusingizemungu alisema yumkini wale wanaoishi juu ya makaburi hayo walikuwa wanajua kilichopo chini ya makaazi yao.

“Ni bahati mbaya kwamba – wakosaji hao, ambao sasa wako huru, hawakujali kuzieleza familia za wahanga mahala yalipo makaburi hayo,” alisema.

Wengi walikuwa makatili, lakini wazuri walikuwepo pia

Ruanda Beisetzung Opfer Völkermord von 1994 (Getty Images/AFP/Y. Chiba)

Watu wakisimama kando na maua yaliowekwa kwenye kaburi la pamoja baada ya kuzikwa kwa majeneza 81 yaliokuwa na mabaki ya wahanga 84,437, Mei 4, 2019.

Akiwa na umri wa miaka saba tu wakati huo, Ingabire anaendelea kustajabu kwamba alinusurika. “Licha ya ukweli kwamba watu wengi walikuwa wakatili, kulikuwepo na wale waliojitia hatarini kuwanusuru wengine,” alisema mama huyo mwenye umri wa miaka 32 sasa.

“Niliokolewa na mwanamke wa Kihutu ambaye alikuwa rafiki mzuri wa mama yangu. Aliniona nakimbia na akanikamata .. hivyo ndivyo nilivyonusurika.”

Umwagaji damu huo wa kikabila ulimalizika Julai 4, baada ya waasi ambao wengi wao walikuwa Watutsi, kuingia mjini Kigali, na kuwatimua wauaji wa kimbari nje ya Rwanda. Jenerali wa waasi alikuwa Paul Kagame, ambae alikuja kuwa rais wa Rwanda, na ameendelea kuwa madarakani tangu wakati huo.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents