Technology

Sababu sita za kwanini wabongo tunapenda Instagram!

Miaka ya hivi karibuni mtandao wa Instagram umeendelea kuwa maarufu zaidi katika ulimwengu wa mitandao ya kijamii. Kwa sasa mtandao huo una watumiaji ‘active’ zaidi ya milioni 300 ambapo zaidi ya milioni 75 huitumia kila siku.

instagram_2787001b

Tayari Instagram imeuzidi mtandao wa Twitter kwa ukuaji wake na miaka sio mingi unaweza kuwa hata zaidi ya Facebook. Good news ni kwamba Instagram ipo chini ya Facebook!

Kwa Afrika Mashariki, Tanzania inaweza ikawa ndio nchi yenye watumiaji wengi zaidi wa Instagram kuliko zingine. Mastaa wa Tanzania pia ndio wanaoongoza kwa kuwa na followers wengi kwenye mtandao huo kuliko wenzao wa Kenya na Uganda.

Kuna sababu nyingi za kwanini Wabongo wametokea kuipenda Instagram na hizi ndio sababu za kufurahisha zinazowafanya waipende zaidi:

1. Kushuhudia vita na matusi ya kati ya Team Nanihii Vs Team Nanihiino

Kwa Tanzania, Instagram kwa sasa ndio mtandao ambao mastaa wanachuma matusi ya kila aina. Na kwakuwa waswahili wanasema akutukanae hakuchagulii tusi, maceleb wetu wanakiona cha mtema kuni. Huko kuna kila aina ya watu ambao wametofautiana malezi na jinsi walivyokuzwa, si ajabu kuona comments nyingi zenye matusi mazito na ya aibu hata kuyasoma kimya kimya.

Matusi mengi yanatokana na upinzani kati ya makundi mbalimbali ya mastaa yenye ushawishi mkubwa nchini. Makundi maarufu yaliyopo kwenye vita vya kila siku ni kati ya Team Wema vs Team Zari na Team Diamond vs Team Alikiba. Ongea kitu kibaya kumhusu Diamond na utaliona joto lake, Team Diamond watakukaba koo. Utatukanwa hadi utamani kuifuta akaunti yako.

Mwandike vibaya Wema Sepetu, Team Wema watakuweka kikaangoni na kukukaanga kwa petrol hadi ujute kuzaliwa.

Muulize TID jinsi Team Alikiba walivyomweka msalabani pale aliposema kuwa ‘Chekecha’ ni wimbo wa kawaida. Usimess kabisa na hizi timu zitakufanya uione dunia chungu.

Kwahiyo wengine tunaipenda Instagram kwa sababu hii tu. Kusoma jinsi mashabiki hawa wanavyoraruana wao kwao wao kwenye post za mastaa wao – kama vile ni ajira waliyopewa.

Haijalishi staa ameweka kitu kibaya ama kizuri, kinachotokea ni kuwa team pinzani huponda tu. Staa mara nyingi hukaa kimya na kuwaacha mashabiki wake wamjibie – hapo ndipo utamu wa Instagram unapokuja. Watabishana, watachambana, watatukanana, wataitana kwa makundi na kutetea upande wao na kumwacha staa akiwa ameweka mguu juu na juice embe pembeni yake, akiangalia TV na huku akicheka tu kusoma ligi hiyo inavyooendelea.

Kwa wengine ligi hiyo ambayo unaweza kuhisi watu hawa wanalipwa, imekuwa ni burudani tu ya kuwepo Instagram. Tunasoma comments, tunalike, tunacheka, siku imepita!

2. Selfies na Fahari ya Macho!

Baadhi ya dada zetu wako mstari wa mbele kupost picha za kuvutia japo zina utata kama nini! Picha za mapaja wazi, picha zinazoonesha figure zao na jinsi ‘walivyo na bright future’ nyuma yao au picha za nazi zao za vifuani. Wasichana wenye desturi ya kupost picha za aina hiyo wana wafuasi wengi.

3. Kuona jinsi Kiingereza kilivyo lugha ngumu kwa wabongo

Kiingereza ni lugha ngumu sana kwa wengi wetu. Wengine tumelikubali hilo na kuamua kutojidhalilisha hadharani kwa kuandika Kiingereza mbofu mbofu. Lakini wengine huamua kuwa wabishi tu na kukiandika kwa uwezo walionao. Hapo ndipo utakutana na sentensi kama ‘You are entering me in the bush’, ‘I am on stage yesterday’, ‘Zanzibar Highland’ na zingine nyingi. Raha sana!

4. Watajuaje kuwa umenunua nguo mpya?

Instagram ni sehemu nzuri ya kushow off kiroho safi. Ni sehemu muhimu ya kutafuta heshima mjini. Hata Mwana FA alisema ‘usiponiheshimu mimi utaheshimu hela zangu’ – ndipo kilichopo Instagram. Ukinunua nguo, cheni, kiatu au gari mpya Instagram ndio sehemu nzuri ya kuumiza roho watu – kama vile Diamond alivyoumiza watu na ‘state house’ yake. Ndio maana wengi tunaipenda. Angalizo: Wakati mwingine maisha ya Instagram si maisha halisi nyuma ya pazia!

5. Kusoma misuto

Le Mutuz, Alberto Msando, Bikira wa Kisukuma na Mr Problem Solved ni mabingwa wa misuto chanya. Hiyo imewasaidia kuvuta followers wengi kwenye akaunti zao.

Le Mutuz amekuwa mstari wa mbele kuwashushua masistaa tu na mabishoo wa mjini ambao ni mabingwa wa maisha ya kifahari kwenye Instagram wakati maisha yao halisi yanatia huruma. Msando ambaye ni mwanasheria maarufu anafahamika kwa ujumbe wake kuhusu kazi, utajiri na ushauri kwa vijana kujituma katika katika kazi zao.

Mr Problem Solved ni bingwa wa kuandika ujumbe unaomsha hasira za kutafuta na kuutafuta ubilionea. Bikira wa Kisukuma kama alivyo Msando naye amebobea katika ‘ushushuzi’. Hao ni baadhi tu ya washushuaji hodari wanaotufanya tuipende Instagram.

6. Kila mtu anaweza kuwa mfanyabiashara

Siku hizi ofisi ya mtu si pale aliposimama peke yake, bali ofisi inaweza kuwa kwenye akaunti ya Instagram. Kuna vijana kibao ambapo wengine hawana hata maduka wala ofisi lakini wanaweza kukufikishia bidhaa mbalimbali nyumbani kwako. Wateja wao ni followers wao. Followers wengi, faida zaidi.

So Instagram ni sehemu ambayo unaweza kuitumia kuondoa stress zako kwa kushuhudia ligi mbalimbali lakini pia inaweza kukuongezea zaidi stress kama ukiamua ‘kustick your nose where it doesn’t belong!

Unangoja nini kuingia Instagram?

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents