Habari

Sababu tano za kuanza kuweka bajeti yako binafsi

Hakuna mtu anayetaka kuwe na bajeti, huo ni ukweli rahisi sana. Kuweka bajeti ya maisha yako ni kazi inayoambatana na vikwazo vinavyosababisha wewe kutopata unachotaka wakati unataka uwe nacho.

budget

Kuna sababu lukuki za watu wengi kwanini hawaweki bajeti ya vitu vyao au matumizi yao ya kila siku. Wengine wakifikiri wao ni maskini hivyo hawahitaji kupanga bajeti ya maisha yao, lakini ukweli ni kwamba bajeti ni kama nguo inayokutosha ambayo inakusaidia kuonekana vizuri hivyo kukufanya kutokuwa na matumizi yasiyokuwa ya lazima hivyo kujikomboa kiuchumi.

Kuna sababu tano ambazo zinakufanya unatakiwa kuanza kutengeneza bajeti yako leo;

1.Unachagua ni lini na jinsi gani ya kutumia pesa

Bajeti inakusaidia namna ya kuamua matumizi yako binafsi ya pesa. Huhitaji kufanya maamuzi magumu kila mwisho wa mwezi kama una bajeti yako. Unapopanga kulingana na umuhimu na vitu vya msingi unavyohitaji, au kiasi gani kuweka kwenye akiba badala ya kuongeza viwalo vingi ili uonekane unakwenda na fasheni kila wakati.

Unapoweza kujua fedha fulani nitaitumia kwenye kitu fulani na kwa mpango fulani inasaidia kuweka mwelekeo wa fedha yako na kujua upunguze wapi ili uongezee sehemu gani katika matumizi yako. Mfano kuna wengine wanaweza kwenda kwenye starehe au kununua viatu kila wiki na mwingine akaamua kuachana na manunuzi ya kila wiki akawa anakula hiyo hela.

Jambo la msingi bajeti inakusaidia kutumia kulingana na kipato chako na inashauriwa matumizi yako yawe chini kuliko kipato chako.

2. Unaacha kuwa na mashaka kuhusu fedha yako

Matatizo ya fedha yako kupotea au kuisha bila kujua hela inaishaje kutaisha. Unapokuwa na bajeti inasaidia kuondoa mawazo ya hela au msongo wa mawazo unaotokana na hela kwani unakuwa unajua hela yako itatumika kwenye nini na nini zaidi ya hapo unatafuta mbadala mwingine. Unapoweka mpango wa matumizi yako mwanzoni mwa mwezi kila mwezi inakusaidia kufika mwisho wa mwezi huku unajua fedha yako itafanya nini na vile vile ni rahisi kufikia malengo yako kuliko kukurupuka katika matumizi ya kila siku.

3. Acha kukopa kila mwezi

Kama umechoka kukopa kila mwezi na kujikuta hela ilishapungua kabla ya kuipokea mwisho wa mwezi wasiwasi wako utaondoka tu pale ambapo utaanza kuweka bajeti na mipango ya matumizi yako kila mwezi. Bajeti itasaidia kufanya manunuzi yako labda kila wiki n.k

4. Ugomvi wa hela unakwisha kabisa

Unapokuwa na bajeti inakupa uwezo wako wa kufanya maamuzi na ukomo wa maamuzi hayo. Unapopanga matumizi na familia yako au na rafiki zako huwezi kwenda zaidi ya bajeti yako ambayo umeweka kwenye mambo ya starehe.

Na kila mtu ana bajeti yake hivyo hakuna kulazimishana au kupelekana kwa spidi wakati unajua wewe unaweza kuishia sehemu fulani na baada ya hapo hufanyi zaidi. Utapunguza ugomvi nyumbani kwako unaohusu pesa kwani watajua bajeti ya mwezi imekaaje na matumizi yanatakiwa kuwaje na zaidi ya hapo wanajua haiwezekani hivyo utaishi wewe na familia yako kulingana na kipato cha bajeti yenu.

5. Fedha itakutumikia na kufanya unachotaka

Bajeti inakupa mamlaka ya kutawala mapato yako na matumizi. Hii inamaanisha kufikia malengo yako haihitaji kuwa na hela nyingi sana bali ni kuweka bajeti ya kila kitu na namna utakavyotekeleza mambo yako.

Inaonekana ni kazi ngumu kwa sababu hatujazoea lakini bajeti ni gurudumu la kusaidia kufikia malengo na kuweza kutawala kinachoingia na kutoka katika kipato chako. Kama utaweza kuacha kutumia zaidi ya kile unachopata na wakati mwingine kuchukua na hata kwenye akiba uliyojiwekea mwenyewe inamaanisha unaenda kwa hatua yenye maendeleo makubwa. Kuna mbinu nyingi za kufikia malengo lakini bajeti yako itakusaidia kufika kule unakotaka kufika.

Awali Mwaisanila

A Personal Career Development specialist, passionate about empowering emerging generations of student, graduates and working class.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents