Moto Hauzimwi
TECNO Spark 2

Sakata la mahujaji hatarini kujirudia

WASIWASI umetanda miongoni mwa mahujaji 1,077 wa Tanzania waliokwenda Makka, Saudia kwa kwenye ibada ya Hijja, wakihofu kutorejea nchini katika wakati muafaka kutokana na kutokuwa na uhakika wa ndege ya kuwasafirisha.

Na Muhibu Said


WASIWASI umetanda miongoni mwa mahujaji 1,077 wa Tanzania waliokwenda Makka, Saudia kwa kwenye ibada ya Hijja, wakihofu kutorejea nchini katika wakati muafaka kutokana na kutokuwa na uhakika wa ndege ya kuwasafirisha.


Habari kutoka Madina, Saudia, ambako mahujaji walielekea jana kwa ajili ya ibada na kutembelea maeneo mbalimbali ya kihistoria, zinaeleza kuwa mahujaji hao wamekumbwa na wasiwasi huo baada ya siku waliyotarajia kuanza kurejea nchini, kutoonekana katika kumbukumbu za mamlaka ya nchi hiyo.


Baadhi ya mahujaji, akiwamo kiongozi wa mahujaji kutoka taasisi ya Tanzania Muslim Hajj Trust ya jijini Dar es Salaam, Alhaj Juma Nchia waliozungumza na mwandishi wa gazeti hili kwa simu kutoka Saudia jana, walithibitisha kuwa na wasiwasi huo.


Ibada ya Hijja kwa mwaka huu, ilikamilika Desemba 22 baada ya mahujaji kutekeleza ibada ya kumpiga mawe shetani katika eneo la Jamarati, lililoko Mina, mjini Makka.


Baada ya kukamilika kwa ibada hiyo, kundi la kwanza la mahujaji hao ambao wiki chache zilizopita walikwama katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam kwa zaidi ya siku kumi na moja kutokana na kukosa ndege ya kuwasafirisha katika muda muafaka, lilitarajiwa kuanza kurejea Desemba 29, wakati kundi la pili lilitarajiwa kurejea nchini siku inayofuatia.


Wote walitarajiwa kurejea nchini na ndege ya kukodiwa na serikali baada ya kuingilia kati safari yao ya kwenda na kurudi Saudi Arabia baada ya mahujaji hao kukwama kuondoka nchini kwa zaidi ya siku kumi na moja.


Hata hivyo, wakati mahujaji hao ambao safri yao ilioratibiwa na baadhi ya taasisi za Kiislamu za Tanzania Bara na Zanzibar wakishikwa na wasiwasi huo, mahujaji 164 walioratibiwa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), wameondolewa wasiwasi, baada ya uongozi wa baraza hilo kuwahakikishia safari yao ya kurejea itakuwa Desemba 31, mwaka huu.


Akizungumza kwa simu kutoka Saudi Arabia jana, Nchia alisema mamlaka ya Saudia inayohusika na usafirishaji, iliwazuia kuondoka nchini humo, baada ya tarehe walizoombewa nafasi ya kusafiri kutokana na kutoonekana katika kumbukumbu za kompyuta za mamlaka hiyo.


Nchia alisema wamekumbana na mkasa huo baada ya kuondoka Makka na kwenda Madina kufuatilia nafasi za safari walizoombewa bila mafanikio.


Alidai kutokana na hali hiyo, walijitahidi kuwasiliana na Ubalozi wa Tanzania nchini humo kuomba msaada, lakini hadi kufikia jana jioni walikuwa hawajapewa ushirikiano wowote.


“Kila tunapojaribu kufuatilia Balozi wetu hapoa anatukwepa hivyo hatujui tutaondoka lini. Tunalazimika kupata huduma zote kwa mashirika yaliyoratibu safari yetu,” alidai Alhaj Sheikh Asbatt ambaye ni mmoja wa mahujaji walioko nchini humo.


Alipoulizwa, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Ndege Tanzania (ATC), Balozi Mustafa Nyang’anyi, alisema hawezi kuzungumzia suala lolote linalohusika na mahujaji na kumtaka mwandishi awasiliane na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Miundombinu, Omar Chambo ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati Maalum ya Serikali ya Kushughulikia Safari ya Mahujaji.


Chambo alipoulizwa, alisema haoni sababu kwa mahujaji hao kuwa na wasiwasi kwani ndege ya kuwarejesha nchini ipo.


Alisema wanachosubiri ni mahujaji hao kupanga siku ya kurejea nchini na kuongeza kuwa siku tatu zilizopita, walituma ujumbe wa watu watatu kwenda Saudi Arabia kushughulikia suala hilo.


“Kule Saudi Arabia tuna Balozi wetu, tumepeleka watu watatu na wamekutana na Balozi. Tutawapelekea ndege. Kazi yetu ni kuhakikisha mahujaji wanarudi nchini,” alisema Chambo.


Wakati hayo yakijiri, Katibu wa Idara ya Hijja na Umra ya Bakwata, Alhaj Swed Twaibu aliliambia gazeti hili juzi kwa simu kutoka Saudia kuwa mahujaji wote walioratibiwa safari hiyo na baraza hilo, wako salama na kwamba wanatarajia kurejea nchini Desemba 31, mwaka huu majira ya saa 4:00 usiku na ndege ya Shirika la Ndege la Yemen (Yamenair).


Alhaj Swed alisema kuanzia juzi walikuwa Madina wakiendelea na ibada.


“Mahujaji wote wako salama, hivi sasa tuko Madina tunaendelea na ibada. Tutarejea tarehe 31 Desemba saa 4:00 usiku na Yemenair…,” alisema Alhaj Swed.


Naye Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Bakwata Taifa, Sheikh Khamis Mataka, ambaye ni mmoja wa viongozi wakuu wa baraza hilo wanaowaongoza mahujaji hao, alimwambia mwandishi wa Mwananchi kwa simu kutoka Saudia jana kuwa wanatarajia kurejea nchini Januari Mosi, mwakani.


“Mahujaji wote wako salama. Hali ya hewa ambayo ni ya baridi na msongamano wa watu, inasababisha mafua, kifua na homa kwa baadhi ya mahujaji,” alisema Sheikh Mataka.


Alisema jambo jana walienda Madina ambako watazulu kaburi la Mtume Muhammad (S.A.W.) na kuswali katika msikiti wake (Mtume Muhammad S.A.W.


“Sala moja katika msikiti huo ni sawa na sala elfu moja zinazosaliwa katika misikiti mingine ukiondoa msikiti mkuu wa Makka,” alisema Sheikh Mataka.


Alisema mbali na kuzuru kaburi hilo, mahujaji pia watatembelea sehemu mbalimbali za kihistoria, likiwemo eneo la makaburi ya Baqii, walikozikwa maswahaba wengi wa Mtume Muhammad (S.A.W.).


“Hakuna muda maalum wa kuwapo Madina kwa kuwa kuwapo Madina ni nje ya ibada ya Hijja ambayo imeshatimia. Wengi hupenda kukaa siku nane angalau wapate jumla ya sala 40 katika msikiti wa Mtume.


Source: Mwananchi

Related Articles

Bongo5

FREE
VIEW